Luhaga Mpina kutimkia ACT na kupewa nafasi kuwania Urais 2025
![]() |
| Viongozi wa ACT Wazalendo wakimkaribisha Ndg. Luhaga Mpina |
Na mwandishi wetu
Mpina amepokelewa na Viongozi Wakubwa wa Chama hicho akiwemo Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu sambamba na Zitto Kabwe, Ado Shaibu na wengine.
Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imempendekeza Luhaga Mpina na Aaron Kalikawe kuwa wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Urais wa Zanzibar.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao maalum kilichofanyika tarehe 5 Agosti 2025, Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema Agosti 06, 2025 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Ndugu Shangwe Ayo, majina yaliyopendekezwa kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Aaron Kalikawe pamoja na Gerson Luhaga Mpina.
Kwa upande wa Urais wa Zanzibar, Halmashauri Kuu imependekeza jina la Ndugu Othman Masoud Othman, ambaye ndiye mwanachama pekee aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo. Othman Masoud Othman pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa majina yote ya wagombea yaliyopendekezwa yatawasilishwa kwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu imepokea na kuridhia uamuzi wa Ndugu Dorothy Jonas Semu, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, wa kujiondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dorothy Semu alieleza Halmashauri Kuu kuwa amefikia hatua hiyo kwa kuzingatia wajibu wake wa kiuongozi, kwa nia ya kukipa nguvu chama katika mapambano ya kisiasa ya kukiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, sambamba na kutazama mazingira halisi ya kisiasa nchini kwa sasa.
![]() |
| Mtiririko wa picha za viongozi mbalimbali wa ACT Wazalendo wakimkaribisha Ndg. Luhaga Mpina |




