Chama cha National League for Democracy (NLD) leo kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2025 hadi 2030.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, amesisitiza dhamira ya NLD kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya Watanzania.
Doyo amesema Ilani hiyo imebeba vipaumbele vinavyogusa maisha ya kila Mtanzania kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi, kijamii na kisiasa nchini.
“Ilani hii inakwenda kutengeneza maisha bora ya kila Mtanzania na kumaliza kero zote zinazowakabili ikiwemo kero kubwa za changamoto ya ajira, sekta ya afya ambabo mama mjamzito anatakiwa kulipa fedha anapojifungua, lakini pia maiti inapaswa kulipiwa deni," amesema Doyo.
Kwamba kama Chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kupitia Ilani hiyo katika Sekta ya Afya watahakikisha mama wajawazito wanajifungua bure na kunakuwa na msamaha wa madeni kwa maiti zote.
Amesisitiza kuwa Ilani hiyo imebeba dira ya matumaini inayolenga kuondoa umasikini, kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii, na kujenga taifa lenye usawa na haki kwa wote.
Kwa uapande wa Katibu wa Kamati ya Uandaaji wa Ilani hiyo Fahadi Hassan Doyo amesema kuwa Ilani hiyo imeundwa kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).