Breaking News

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA WABUNGE KWENYE MICHEZO





Na. Wellu Mtaki, Dodoma 


Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wabunge kwani  inatambua mchango mkubwa wa Bunge katika kuimarisha umoja wa kitaifa kupitia michezo.


Kauli hiyo ameitoa waziriMkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akiongoza mamia ya wabunge, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali kufunga rasmi Bonanza Maalum la Bunge maarufu kama Grand Bunge Bonanza, lililofanyika jijini Dodoma ikiwa ni bonanza la mwisho kwa Bunge la 12.


“Kwa miaka mitano mfululizo Grand Bunge Bonanza limekuwa jukwaa la kuhamasisha mazoezi na maisha bora. Faida zake ni pana kutoka kwa wabunge, wafanyakazi wa Bunge hadi kwa wananchi wa kawaida,” alisema Majaliwa.

"Bonanza hilo la mwisho kwa Bunge la 12 limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, na riadha. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ni “Michezo kwa Afya, Umoja na Maendeleo.”





Naye Naibu Spika, Mussa Zungu ametambua mchango wa CRDB katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule kubwa katika Wilaya ya Ilala, jambo lililopongezwa. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bonanza hilo ambaye pia ni Mbunge wa Makete, Festo Sanga, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhamasisha michezo, akisema michezo si afya pekee bali pia ni ajira na njia ya kujenga mshikamano wa kitaifa.

“Bonanza hili limekuwa chachu ya mshikamano, afya ya mwili na akili, na hata kutengeneza marafiki kati ya wabunge, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla,” alisema Sanga.

Akitoa salamu katika wiki ya kuzuia madawa ya kulevya  mwakilishi kutoka Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali Aretas James Lyimo amesema bonanza hilo limekuja wakati muafaka wa kuadhimisha wiki ya kupambana na dawa za kulevya, akieleza kuwa dawa hizo ni tishio kwa uchumi na mustakabali wa vijana wa taifa.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Msekela, amesema benki hiyo inajivunia kuwa mdau wa kudumu wa bonanza hilo, akisisitiza kuwa wamekuwa wakishirikiana na wabunge hata katika kuendeleza miradi kwenye majimbo yao.