GESI ASILIA INAMCHANGO MKUBWA KATIKA MAENDELEO YA JAMII
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeeleza kuwa sekta ya gesi asilia imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na kusaidia katika jitihada za kulinda mazingira nchini.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya sekta hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa PURA, Mhandisi Charles Nyange, amesema uwekezaji katika gesi asilia unaendelea kukua kwa kasi, huku matumizi ya nishati hiyo yakishika kasi katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam.
"Kutokana na umuhimu wa gesi asilia hasa kwa matumizi ya majumbani, PURA inaendelea na juhudi za kusambaza miundombinu ya gesi hiyo kadri rasilimali fedha zinavyopatikana," amesema Mhandisi Nyange.
Ameongeza kuwa tayari baadhi ya Watanzania wamenufaika kupitia ajira za muda na ajira za kudumu zinazotokana na shughuli za gesi asilia, hatua inayosaidia kuinua kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya ndani.
Aidha, PURA inalenga kuwajengea uwezo Watanzania na kampuni za ndani ili washiriki kikamilifu katika miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
"Malengo yetu mengine ni kuhamasisha uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, kuwafikia wananchi kwa awamu na kukuza fursa za ajira," amesema Mhandisi Nyange.
PURA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinatumika kwa manufaa ya Taifa na kuwanufaisha Watanzania kupitia ushiriki wa moja kwa moja na wa kimkakati katika sekta hiyo muhimu
