Breaking News

MHE. RAIS ANATARAJIWA KUWA MGENI RASMI KWENYE BONANZA LA BUNGE.



Wellu Mtaki, Dodoma 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Bunge, linalotarajiwa kufanyika Juni 21, 2025 kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari John Merin, Miyuji jijini Dodoma.


Bonanza hilo ambalo limepewa kaulimbiu “Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Maendeleo ya Taifa,” linaandaliwa kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, na linalenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.


Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mwenyekiti wa Bonanza la Bunge, Mheshimiwa Festo Sanga, amesema kuwa Bonanza hilo ni sehemu ya kuhitimisha shughuli za Bunge kwa kipindi cha miaka mitano, na pia kuwaunganisha wabunge, wananchi na wadau kupitia michezo na burudani zenye ujumbe wa amani, mshikamano na demokrasia.


Bonanza la mwaka huu ni kubwa na la kipekee kwa sababu linahitimisha kipindi cha Bunge na linafungua ukurasa mpya kuelekea uchaguzi. Tunamshukuru Rais kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kuwa sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi,” alisema Sanga.


pia amefafanua kuwa michezo itakayochezwa  itakuwa ni mpira wa miguu, pete, kikapu, mpira wa wavu na kuvuta kamba pamoja na  kutakuwa na matembezi ya hiari yatakayoanzia Chuo cha Mipango hadi viwanja vya bonanza ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mazoezi na afya bora.


Benki ya CRDB ambayo ni mdhamini mkuu wa bonanza hilo, imetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 130. Mwakilishi wa benki hiyo, Ntully Mwambapa, alisema kuwa CRDB itaendelea kushirikiana na Bunge kuandaa matukio ya kijamii na kimaendeleo yanayolenga afya, mshikamano na ustawi wa wananchi.