BAT Yabaini Dawa za Tiba Asili Zenye Kasoro Sokoni, Yatoa Onyo kwa Wananchi
Na Mwandishi Wetu-Dodoma
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala (BAT) Prof. Joseph Otieno limewaonya wananchi kuwa waangalifu wanapotumia dawa za tiba asili kutokana na kubainika kwa baadhi ya bidhaa zenye kasoro ambazo zinaweza kuhatarisha afya na usalama wa watumiaji. Baraza hilo limesema pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya tiba asili nchini, bado kuna changamoto ya uwepo wa dawa zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Juni 5,2026 Prof.Joseph Otieno amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 walifanya zoezi la ufuatiliaji wa dawa za tiba asili sokoni katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam. Ufuatiliaji huo ulibaini baadhi ya dawa kuwa na mapungufu katika vifungashio, taarifa za lebo, ujazo pamoja na muda wa matumizi.
Baraza hilo lilibainisha kuwa dawa moja ya asili iitwayo Joy ilikutwa kuwa na sumu katika kiwango kisichokubalika. Kwa mujibu wa BAT, hali hiyo inaashiria kutokuzingatiwa kwa viwango bora vya uzalishaji na uhifadhi wa dawa, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu.
Aidha, BAT imeeleza kuwa matumizi ya dawa yenye kiwango kikubwa cha sumu yanaweza kuongeza hatari ya kupata saratani, kuharibu ini na figo pamoja na kusababisha madhara mengine ya muda mrefu kwa mwili wa binadamu.
Katika hatua nyingine, dawa mbili za tiba asili zilibainika kuchanganywa na kemikali za dawa za kisasa ambazo hazikuainishwa kwenye lebo za bidhaa hizo.
Uchunguzi uliofanywa umeonesha kuwa baadhi ya wazalishaji wamekuwa wakiongeza dawa za kisasa kwenye bidhaa za tiba asili kinyume cha sheria, hali inayotajwa kuwa tishio kwa afya ya jamii.
Miongoni mwa dawa zilizobainika kufanya hivyo ni Powaful Banana Medicine ambayo ilibadilishwa kuwa Banana Medicine, na kutangazwa kuwa dawa ya kuongeza nguvu za kiume. BAT imesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukiuka taratibu na sheria zinazosimamia huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
Baraza hilo limewataka wananchi kuhakikisha wanatumia dawa za tiba asili zilizosajiliwa na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu husika kabla ya matumizi, huku likisisitiza kuwa dawa zote zinapaswa kufanyiwa tathmini ya ubora, usalama na ufanisi kabla ya kuruhusiwa kuuzwa na kutumika nchini.

