Breaking News

CHAMA CHA BIBLIA TANZANIA CHA SAMBAZA MAANDIKO ZAIDI YA LAKI TANO MWAKA 2025

 .


Na Wellu Mtaki, Dodoma

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Biblia Tanzania, Askofu Dkt. Mark Malwa Malekana amesema kuwa katika mwaka 2025 chama hicho kimefanikiwa kusambaza jumla ya maandiko 538,544, ikilinganishwa na maandiko 512,650 yaliyosambazwa mwaka 2024.Amesema maandiko hayo yamesambazwa kupitia mifumo na lugha mbalimbali ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Askofu Malekana ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa 40 wa Chama cha Biblia Tanzania. Ameeleza kuwa chama hicho kimeendelea kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kueneza Neno la Mungu nchini.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Bible Plaza, maandalizi ya Kamusi ya Biblia, Itifaki ya Biblia pamoja na uchapishaji wa kitabu cha historia ya Chama cha Biblia Tanzania. Pia chama hicho kimefanikiwa kuzindua Biblia za lugha za Kikagulu na Kihehe kwa lengo la kuwafikia waumini wanaotumia lugha hizo za asili.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Biblia Tanzania, Dkt. Alfred Elias Kimonge amesema chama hicho kimeendelea kuwahudumia watu wenye ulemavu wa macho kwa kuwapatia Biblia za Nukta Nundu pamoja na mafunzo ya uponyaji wa majeraha ya nafsi (Trauma Healing) kwa jamii zinazokumbwa na changamoto mbalimbali za maisha.

Dkt. Kimonge ameongeza kuwa katika mwaka 2025 chama hicho kimeendelea kutekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake na wasichana zaidi ya 3,200 pamoja na wanaume wanaonufaika na mpango huo katika wilaya za Gairo na Kilosa. Amesema lengo la mradi huo ni kutoa elimu na kuwawezesha wananchi waliokosa fursa ya masomo kutokana na sababu mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Aidha, viongozi wa chama hicho wamewataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kueneza maandiko matakatifu pamoja na kusaidia makundi maalumu yenye uhitaji wa elimu ya kiroho na kijamii. Wamesema ushirikiano huo utasaidia kufikia jamii nyingi zaidi hasa maeneo ya vijijini.

Katika mkutano huo, wajumbe mbalimbali walipata nafasi ya kujadili mafanikio, changamoto na mipango ya maendeleo ya chama hicho kwa miaka ijayo. Baadhi ya wajumbe wamepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa chama katika kuhakikisha huduma za Biblia zinawafikia Watanzania wa rika zote.

Vilevile, Chama cha Biblia Tanzania kimeeleza dhamira yake ya kuendelea kutumia teknolojia ya kisasa katika usambazaji wa maandiko na mafunzo mbalimbali ya kiroho. Hatua hiyo inalenga kuwafikia vijana na makundi mengine kupitia mifumo ya kidigitali inayorahisisha upatikanaji wa Biblia na mafunzo yake.

Mkutano Mkuu wa 40 wa Chama cha Biblia Tanzania umehudhuriwa na viongozi wa dini, wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na wadau wa maendeleo waliojadili namna ya kuimarisha huduma za kiroho na kijamii kwa manufaa ya jamii ya Watanzania.