Breaking News

vijana 521 waondoka kwa ajira nje ya nchi

 


Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Patrick Kawogo, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya kutafuta ajira nje ya nchi, amesema vijana wanaopata fursa za ajira kimataifa wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia ujuzi na kipato watakachopata.

Amesema kampuni yake inaendelea kuwaunganisha vijana na fursa za ajira pamoja na mafunzo ya kazi katika nchi mbalimbali duniani, zikiwemo Marekani, Canada na baadhi ya nchi za Scandinavia kama Ujerumani, Norway, Denmark na Uholanzi.

Kadhalika, ameeleza kuwa mafunzo wanayowaandalia vijana hao huchukua kipindi cha mwaka mmoja au zaidi, yakijikita katika sekta za kilimo, utalii (tourism and hospitality) pamoja na uhandisi, ambazo zina mahitaji makubwa ya ajira kimataifa.

Amesisitiza kuwa fursa hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa vijana wa Kitanzania, hasa katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira nchini.

Awali, akizungumza katika hafla ya kuwaaga vijana 521 waliopata ajira nje ya nchi iliyofanyika Machi 27, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mheshimiwa Deus Sangu, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza ajira kwa vijana.

Alisema Serikali inaendelea kufungua na kuimarisha njia salama za uhamiaji wa nguvu kazi kwa kushirikiana na nchi rafiki pamoja na taasisi za kikanda na kimataifa ili kuhakikisha Watanzania wanapata ajira zenye staha, kulindwa haki zao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia.

Aidha, aliwahakikishia vijana hao kuwa Serikali imejipanga kulinda usalama wao wanapokuwa nje ya nchi, akiwataka waende kwa utulivu na kujiamini wakijua kuwa Serikali ipo pamoja nao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ajira, Bi. Jane Sologo, aliwashukuru mawakala binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kuwaunganisha Watanzania na ajira za nje.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala Tanzania, Bw. Abdallah Khaled Mohamed, aliipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na mawakala hao, akisema umeongeza ufanisi na uaminifu katika usimamizi wa ajira za nje.