Breaking News

Serikali yahakikishia akiba ya mafuta hadi julai licha ya mvutano wa mashariki ya kati




Na Hawa ismail – dar es salaam

Serikali imehakikisha kuwa Tanzania ina akiba ya kutosha ya mafuta hadi mwezi Julai mwaka huu, hatua inayolenga kuondoa hofu ya uhaba licha ya changamoto za usambazaji zinazosababishwa na mvutano wa kimataifa, hususan katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unabaki imara kwa miezi kadhaa ijayo, kufuatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa mapema kudhibiti athari za mabadiliko ya soko la dunia.

Dk. Mataragio ameeleza kuwa mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati umechangia kupanda kwa gharama za usafirishaji na changamoto katika upatikanaji wa mafuta, lakini Tanzania imeweza kujipanga vyema kukabiliana na hali hiyo.

Amesema kabla ya kufanya ziara katika maghala ya kuhifadhi mafuta (stock depots), Serikali ilifanya tathmini ya kina na kujiridhisha kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta nchini ni tulivu na ya kuridhisha.

“Kwa sasa Serikali imejipanga kuwa na akiba ya mafuta hadi mwezi Julai. Hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu, mafuta yapo ya kutosha,” amesema Dk. Mataragio.

Ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa taarifa za ucheleweshaji wa baadhi ya malori kupakia mafuta pamoja na changamoto za vibali, mifumo ya usambazaji inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi bila kuathiri upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Camel Oil, Saleh Bajber, amesema kampuni hiyo inaendelea kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta na imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha upatikanaji hauyumbi.

Amesema Camel Oil imeagiza zaidi ya lita milioni 70 kwa matumizi yake pamoja na lita milioni 84 kwa mtandao wake wa usambazaji, huku tayari ikiwa imesambaza lita milioni 44 ndani ya mwezi huu.

“Hadi sasa tunazo zaidi ya lita milioni tano na mauzo yameongezeka, hali inayoweza kuwa imesababishwa na wananchi kuongeza manunuzi kutokana na hofu ya upungufu,” amesema Bajber.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dk. James Andilile, amesema hali ya soko la dunia imeathiri upatikanaji wa mafuta kutokana na utegemezi mkubwa wa nchi nyingi kutoka Mashariki ya Kati.

“Upatikanaji wa mafuta duniani umekuwa changamoto kutokana na hali ya Mashariki ya Kati, lakini Tanzania tulishachukua hatua mapema hivyo hatuna shida ya mafuta kwa sasa,” amesema Dk. Andilile.

Ameongeza kuwa EWURA inaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la mafuta kila siku ili kuhakikisha usalama wa nishati hiyo pamoja na kudhibiti bei kwa watumiaji.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wasambazaji wa Mafuta nchini (TAPSOA), Augustino Mmasi, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo umeimarisha upatikanaji wa mafuta nchini.

“Nawafahamisha wafanyabiashara na wananchi kuwa mafuta yapo ya kutosha. Tumeendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha usambazaji unakuwa wa uhakika,” amesema Mmasi.

Hata hivyo, ameonya kuwa gharama za usafirishaji zinaweza kuongezeka kutokana na hali ya soko la dunia, jambo linaloweza kuathiri bei za mafuta katika siku zijazo.

Pamoja na changamoto hizo, Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa wingi na kwa bei himilivu, huku ikiwataka wananchi kuendelea kununua mafuta kwa matumizi ya kawaida bila kuwa na hofu ya upungufu.