Breaking News

CRC YADAIWA BILIONI 4.7 NA TRA,MALI ZAKE ZIKISUBIRI KUPIGWA MNADA KUFIDIA DENI LA BENKI LA BILIONI 26.

 

Na. Mwandishi wetu,

Mamlaka ya mapato Tanzania, TRA inaidai zaidi ya shilingi bilioni 4.7 kama malimbikizo ya kodi kampuni ya Continental Reliable Clearling (CRC), fedha ambazo kampuni hiyo imezichepusha kwa matumizi binafsi badala ya kulipa kodi ya Watanzania 

Hii inaibuka ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kampuni hiyo ya CRC kugonga mwamba kuitumia Mahakama Kuu ya Tanzania kama kichaka cha kukwepa kulipa madeni, kwa mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya kampuni hiyo iliyoyapeleka dhidi ya benki za Equity Kenya na Tanzania na kuiagiza kampuni hiyo kulipa madeni waliyokopa na kuacha ujanja ujanja.

Kufuatia uamuzi huo, tangazo la mnada wa mali za kampuni hiyo lililotolewa katika magazeti ya Mwananchi na The Citizen ya tarehe 19 mwezi wa pili kupitia kampuni ya udalali ya Adili Auction Mart Limited, lilithibitisha kuwa mali za CRC zinakwenda kuuzwa ili kufidia deni la benki linalofikia Shilingi bilioni 26.

Hata hivyo, wakati harakati za mnada huo wa njia ya zabuni uliopangwa kufungwa  Machi 9 mwaka huu zikiendelea, TRA imeibuka na kubainisha kuwa inaidai kampuni hiyo Shilingi bilioni 4.7 za malimbikizo ya kodi fedha za Watanzania zilizopaswa kwenda kwenye shughuli za maendeleo.

Katika barua waliyonakiliwa kampuni ya CRC ikielekezwa kwa Mkurugenzi wa Adili Auction Mart, TRA imeeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, dalali huyo anatambuliwa kama wakala wa kuhakikisha kiasi hicho cha kodi kinalipwa mara tu baada ya kufanyika kwa mnada huo.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya fedha, hali hiyo inaonesha namna ambavyo Mahakama inavyotakiwa kuendelea kuwa macho kwenye kuwadhibiti wafanyabiashara wanaokwenda kukopa na kukimbilia mahakamani kutaka kukwepa kulipa madeni kitendo kinachoichafua sekta ya fedha nchini na kudumaza mzunguko wa fedha.


Wanasema mwenendo huo husababisha hasara kwa mabenki na kuwafanya wajasiriamali wadogo kukosa mikopo ambayo kama wangepata ingesaidia kuinua uchumi wa jamii kubwa.

Kwa sasa, CRC inajikuta katikati ya mzigo wa madeni yanayozidi Shilingi bilioni 30 bilioni 26 za benki na bilioni 4.7 za kodi huku macho ya wadau wa sekta ya fedha yakielekezwa kwenye mnada huo wa mtindo wa zabuni unaotarajiwa kuamua hatima ya kampuni hiyo pamoja na mgawanyo wa fedha zinazodaiwa.