WATUHUMIWA 46 MBARONI -MULIRO.
Na Mwandishi wetu Dar es salaam.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam,SACP Muliro Jumanne Muliro amesema jeshi la polisi limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuzuia na kupambana na vitendo vya kihalifu, huku likihakikishia wananchi kuwa hali ya usalama jijini ni shwari.
Jeshi hilo limewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa muhimu zinazosaidia kudhibiti uhalifu, hatua inayochangia kulinda amani na usalama wa jiji Hilo.
Katika kipindi cha kuanzia Januari 30 hadi Februari 24, 2026, Jeshi la Polisi Tanzania Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata jumla ya watuhumiwa 46 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya kijinai.
Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24,2026 ambapo amesema miongoni mwa makosa hayo ni unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji wa nyumba na maghala (godown), pamoja na wizi wa mali za umma na binafsi.
Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum SACP Muliro Jumanne Muliro amebainisha kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitumia pikipiki na silaha za jadi kama vile mapanga kutekeleza uhalifu, hususan maeneo ya pembezoni mwa jiji
Amesema wapo waliokuwa wakijihusisha na kuvunja nyumba mchana na usiku na kuiba vifaa mbalimbali, huku wengine wakihusika na kununua na kuuza mali za wizi.
"Jeshi la polisi limekamata pikipiki zaidi ya 20, simu 110, runinga, redio na vifaa vingine vya kielektroniki. Pia zimekamatwa funguo maalum zenye uwezo wa kufungua kufuli aina mbalimbali pamoja na gari kwenye usajili T 457 CQF aina ya Toyota Noah lililokuwa likitumika kusafirisha mali za wizi" amesema Muliro.
Aidha Kamanda Muliro amewaorodhesha watuhumiwa waliokamatwa nao ni Rashidi Mtunguja maarufu “Msamba” na wenzake wanne ambapo walikamatwa maeneo ya Jangwani, Issa Nasoro Kurukutu na wenzake wawili walikamatwa maeneo ya Gongo la Mboto, pamoja na Nicholas Abdallah Said mkazi wa Manzese.
Hata hivyo jeshi limeeleza kuwa ufuatiliaji unaendelea ili kuwakamata wahusika wote kabla au baada ya kutekeleza uhalifu, sambamba na kuzingatia misingi ya kisheria ikiwemo kukusanya ushahidi, ili wapelekwe Ofisi ya Mashitaka na hatimaye mahakamani.
Katika hatua za kisheria zilizochukuliwa Muliro amesema, baadhi ya watuhumiwa wamehukumiwa vifungo vikali ikiwemo kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ubakaji wa kundi na unyang’anyi wa kutumia silaha. Miongoni mwao ni Mwita Marwa na wenzake wawili waliopatikana na hatia Mahakama ya Kigamboni, Adam Samiro aliyehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, pamoja na Jafari wa Chang’ombe na Omari Omari wa Mbande waliopata adhabu kali Mahakama ya Temeke.
Kwa upande wa usalama barabarani, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, hususani wanaopita kwenye barabara za mwendo kasi. Jumla ya madereva 250 walikamatwa katika kipindi hicho, wakiwemo bodaboda 167, bajaji 19 na magari 64, hatua iliyolenga kupunguza ajali na kero kwa watumiaji wa barabara.
Jeshi limewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na kuahidi kuendelea kulinda usalama ili shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani.





