MBOGO TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI KWA KUMTANGAZA KINARA YA SEKTA YA MIFUGO AFRICA
Na Mwandishi wetu
Katika maadhimisho ya *Siku ya Mwanamke Duniani*, kampuni ya Mbogo Tanzania imechukua hatua mahsusi kwa kumtambua na kumuenzi mmoja wa washirika wake muhimu katika sekta ya mifugo na wanyamapori, *Martenique Scott*, kama sehemu ya kuhamasisha uongozi wa wanawake katika kilimo na biashara za kimataifa.
Mbogo Tanzania, kupitia ushiriki wake katika maandalizi ya *Tri Nations Livestock Expo*, imemtambua Martenique kama mfano wa mwanamke anayevunja vikwazo katika sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume.
Martenique ni mmiliki na Mkurugenzi wa kampuni ya *Real Time Agri*, ambayo ni mshirika wa Mbogo Tanzania katika kuandaa Maonesho MAKUBWA pamoja na Mnada wa KIMATAIFA wa Tri Nations Livestock Expo. Kupitia kampuni hiyo, ameunganisha kwa mafanikio masoko ya mifugo na wanyamapori, akileta mtazamo wa kimataifa katika biashara na minada ya kisasa barani Afrika.
Akizungumzia ushirikiano huo, Mkurugenzi wa Mbogo Tanzania, Naweed Mulla anasema mchango wa Martenique umeongeza thamani katika maandalizi ya maonesho hayo, hasa katika kuvutia wawekezaji, wafugaji na wanunuzi kutoka masoko ya nje. Uzoefu wake katika uwakala wa wanyamapori na biashara ya kimataifa umeleta fursa mpya kwa wafugaji wa Afrika Mashariki na Kusini kuingia katika soko la dunia.
Mbogo Tanzania imesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamelenga si tu kusherehekea mchango wa wanawake, bali pia kuonyesha kwa vitendo kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika kuongoza mageuzi ya sekta ya kilimo na mifugo.
Kwa kumtambua Martenique, Mbogo Tanzania imetuma ujumbe wazi kuwa ushirikiano wao unajengwa juu ya maono ya pamoja — kukuza mifugo ya Afrika, kuimarisha minada ya kimataifa na kuweka misingi imara ya biashara endelevu.
Katika kipindi ambacho dunia inaadhimisha mchango wa wanawake katika maendeleo, hatua ya Mbogo Tanzania inaweka mfano wa namna sekta binafsi inavyoweza kutumia majukwaa yake kuhamasisha usawa, uongozi na uwezeshaji wa wanawake katika uchumi wa kilimo.
Maonesho ya Tri Nations Livestock Expo yanatarajiwa kuendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha masoko, kukuza mifugo bora na kufungua milango ya biashara za kimataifa yatafanyika Ubena Zomozi Chalinze tarehe 19 Hadi 21 June, 2026 huku wanawake wakichukua nafasi yao ya mbele katika safari hiyo kupitia tuzo zilizozinduliwa kwenye hafla ya utiaji Saini kati ya NMB Bank na Mbogo Tanzania hivi katribuni kwenye shamba la Ubena litakalo hodhi Maonyesho hayo.
Aidha Mkurugenzi wa Mbogo Tanzania Naweed Mulla alisema Maonesho haya mwaka huu yatatambua juhudi za Wanawake katika kilimo na ufugaji kwa kutoa tuzo za Heshima Tri-Nations women of the year in Agriculture award, tuzo hizi zitaangazia kwenye kilimo na ufugaji.


