Mwanamitindo Miriam Odemba asherehekea siku ya kuzaliwa na watoto wenye mahitaji maalum Dar es Salaam
Dar es Salaam, Februari 19, 2026 — Mwanamitindo wa kimataifa, Miriam Odemba, ameahidi kuendelea kutoa msaada na zawadi kwa watoto wenye mahitaji maalum huku akiwahamasisha kuamini ndoto zao na kuthamini uwezo wao binafsi.
Odemba alitoa kauli hiyo kwa njia ya simu wakati akisherehekea siku yake ya kuzaliwa jijini Dar es Salaam, ambapo aliungana na watoto wa Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu katika hafla maalum ya kusherehekea pamoja nao. Katika maadhimisho hayo, watoto walipata fursa ya kushiriki chakula cha pamoja pamoja na shughuli za kijamii zilizoandaliwa na taasisi yake.
Katika hafla hiyo, makamu mkuu wa shule hiyo, Jacob Mrope, alimkabidhi Odemba tuzo maalum iliyosomeka: *“Tuzo maalum ya kuthamini mchango mkubwa kwako kama ishara ya kuthamini watu wenye ulemavu na mahitaji maalum.”*
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mrope aliishukuru Miriam Odemba Foundation kwa kuendelea kuikumbuka shule hiyo mara kwa mara kupitia misaada na programu za kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Alisema taasisi hiyo imekuwa chachu ya kuwapa watoto matumaini kwa kuwaelimisha kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia mafanikio yao maishani.
“Kitendo cha kuchagua kusherehekea miaka 44 ya kuzaliwa pamoja na watoto hawa ni mfano wa huruma na mshikamano wa kijamii. Kwa niaba ya uongozi wa Jeshi la Wokovu tunawashukuru na tunathibitisha watoto wamefurahi sana na wamemuombea mafanikio mema,” alisema Mrope.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Jenipher Mteleke, alisema uamuzi wa kusherehekea siku ya kuzaliwa katika shule hiyo ulilenga kuonesha upendo na kuikumbusha jamii umuhimu wa kulijali kundi la watoto wenye mahitaji maalum na wenye ulemavu.
Alieleza kuwa taasisi hiyo inalenga kusaidia watoto wenye uhitaji huku ikitoa kipaumbele kwa makundi ambayo mara nyingi husahaulika katika jamii.
“Tunapoendelea kuwafikia watu wenye uhitaji tunaona namna Mungu anavyoweza kubariki maisha yetu. Ndiyo maana tumeona ni muhimu kushirikiana na watoto hawa pamoja na wadau mbalimbali ili kusherehekea nao na kuwapa furaha,” alisema Mteleke.
Taasisi ya Miriam Odemba Foundation imejikita zaidi katika kuwawezesha vijana, hususan wasichana, kupitia kukuza vipaji, elimu ya utamaduni na programu za maendeleo ya kijamii.
Naye mwanafunzi wa shule hiyo, Rahma Moshi, alimshukuru Odemba kwa kuonesha upendo na kujali watoto wenye mahitaji maalum, akisema ujio wake umeongeza faraja na motisha kwa wanafunzi hao.
![]() |




