Breaking News

Waumini 100 Wasilisha Malalamiko Vatican Dhidi ya Viongozi Wakuu wa Kanisa Katoliki Tanzania

 



Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

Mnamo Januari 5, 2026, kundi la waumini wa Kanisa Katoliki wapatao 100 limewasili katika Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania kwa lengo la kuwasilisha barua rasmi ya malalamiko dhidi ya viongozi wawili waandamizi wa kanisa hilo.

Malalamiko hayo yameelekezwa kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima.

Kwa mujibu wa waumini hao, hatua yao imechochewa na kutoridhishwa kwao na maudhui ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Ruwa’ichi wakati wa Misa ya Krismasi iliyofanyika Desemba 25, 2025. Wamedai kuwa mahubiri hayo yalijaa lugha ya ukali, vitisho na hukumu, badala ya kuakisi ujumbe wa faraja, matumaini na upendo unaotarajiwa kutoka kwa viongozi wa kiroho.

Aidha, waumini hao wamesema kuwa mimbari ilitumika kama jukwaa la kuwashambulia wale waliowahi kuwasilisha hoja zao kwa Balozi wa Vatican awali, jambo ambalo wamelitafsiri kuwa ni kinyume na maadili ya kichungaji na haki ya waumini kutoa maoni yao ndani ya kanisa.

Katika malalamiko hayo, Padri Dkt. Charles Kitima naye ametajwa kwa madai ya kujiingiza katika masuala ya kisiasa, hatua ambayo waumini hao wanaona kuwa inakiuka misingi ya utumishi wa kiroho na kuathiri taswira ya kanisa mbele ya waumini na jamii kwa ujumla.