DIWANI KATA YA MAKANGARAWE ATOA MSAADA WA VIFAA VYA SHULE KWA WATOTO WENYE UHITAJI
Na Hawa Ismail – Dar es Salaam
Diwani wa Kata ya Makangarawe, Mhe. Fadhili Mboga, ameendelea kuonesha moyo wa huruma na kujitolea kwa kushiriki katika zoezi la utoaji wa misaada kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. walinufaika na msaada huo uliotolewa kupitia Jumuiya ya Majumuati ya Kiislamu iliyopo katika kata hiyo, wilayani Temeke.
Akizungumza katika tukio hilo leo Januari 03,2026 Diwani Mboga alieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na jumuiya hiyo kwa kujenga kituo maalum cha kulelea watoto yatima katika kata hiyo, ili kuwawezesha kupata huduma muhimu kwa urahisi zaidi.
“Serikali yetu inatambua mchango mkubwa wa dini ya Kiislamu katika jamii. Nimeahidi kuwa katika shule zitakazojengwa, masomo ya dini yatapewa kipaumbele, sambamba na kuboresha vipindi vya dini katika shule za Jitihada na Dovya,” alisema Mboga.
Aidha, aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuchangia fedha kwa ajili ya kuinua dini ya Kiislamu na kuhakikisha maendeleo ya kijamii katika Kata ya Makangarawe yanaimarika kwa pamoja.
Kwa upande wake, Mariam Hamisi, mwanafunzi kutoka Jumuiya ya Majumuati ya Kiislamu ya Masjid Jamiya, alisema kuwa jumuiya hiyo imekuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kuchangia watoto yatima na watu wasiojiweza.
“Leo kama wana Majumuati, tumetoa misaada ya madaftari, mabegi ya shule, penseli, chakula na huduma za afya kwa watoto wanaohitaji,” alisema Mariam.
Mratibu wa elimu ya dini ya Kiislamu Wilaya ya Kisarawe, Sheikh Salum, alisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto, akieleza kuwa elimu ya Qur’an ni msingi imara wa maadili mema. Alipendekeza watoto wapate fursa ya kusoma Qur’an hata nje ya muda wa kawaida wa masomo.
Katika hatua nyingine, Imamu wa Msikiti wa Jamiya Shekh Habibu alitoa wito kwa waumini na wanajamii kushiriki harambee ya kuchangia mfuko wa Wanajamiati kwa ajili ya kusaidia watoto yatima ifikapo mwaka 2027.









