Breaking News

Wamachinga, Bodaboda na Bajaji Kuungana Katika Kongamano Kubwa la Kitaifa Januari 2026

 


Na Hawa Ismail - Dar es Salaam 

Chama cha Wamachinga Tanzania kwa kushirikiana na waendesha bodaboda na bajaji kimetangaza maandalizi ya kongamano kubwa la kitaifa linalotarajiwa kufanyika Januari 2026. Lengo kuu la kongamano hilo ni kujenga ushirikiano wa pamoja katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wajasiriamali wadogo nchini, hususan katika sekta ya biashara ndogondogo na usafirishaji wa abiria.

Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa viongozi wa chama hicho alieleza kuwa kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wakuu wa serikali, taasisi za kifedha, na mashirika ya kiraia. Katika mkutano huo, changamoto za wamachinga, bodaboda na bajaji zitawasilishwa moja kwa moja kwa mamlaka husika ili zipatiwe majibu ya haraka na ya kudumu.

“Kongamano hili litakuwa jukwaa la wazi la majadiliano, siyo tu kwa ajili ya kueleza matatizo, bali pia kutafuta njia bora za kuyatatua kwa njia ya maelewano na ushirikiano wa kweli,” alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania, Ernest Masanja, aliwapongeza wamachinga na mama lishe kwa kuonesha uzalendo na uvumilivu kwa kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Desemba 9 na 25. Alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kulinda amani na utulivu wa taifa, huku akisisitiza kuwa njia bora ya kutatua changamoto ni kupitia mazungumzo na siyo migogoro.

Masanja alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wamachinga, ikiwemo ukosefu wa mikopo kwa wakati, hali inayowakwamisha kupanua biashara zao. Alitoa wito kwa serikali na taasisi za kifedha kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inawafikia walengwa kwa wakati ili kusaidia kuinua uchumi wa vijana na familia zao.

Katika hatua nyingine, mmoja wa viongozi wa waendesha bodaboda alieleza kuwa madereva wengi hulazimika kukaa muda mrefu juani wakisubiri wateja kutokana na ukosefu wa maeneo rasmi ya kupumzikia. Alitoa wito kwa serikali kuboresha miundombinu kwa kujenga vituo vya kisasa vitakavyowasaidia kufanya kazi katika mazingira bora na salama.

Aidha, viongozi hao waligusia fursa za mikopo kwa vijana, wanawake na makundi maalum zilizoidhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Walisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwazi na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinawafikia walengwa waliokusudiwa kwa ufanisi.

Kuhusu migogoro kati ya wamachinga na askari mgambo katika baadhi ya maeneo, Masanja aliiomba serikali kuwatafutia mgambo hao ajira rasmi. Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro na kuongeza amani katika maeneo ya biashara, hivyo kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wajasiriamali wadogo.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kitaifa litakalowakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kazi, kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo ya wamachinga, bodaboda na bajaji nchini.