Wajasiriamali Wajitokeza Kuhamasisha Gen Z Kulinda Amani na Mshikamano wa Kitaifa
Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Wajasiriamali nchini wameeleza dhamira yao ya kuendelea kuwahamasisha vijana wa kizazi cha Gen Z kutambua nafasi yao kama nguvu kazi muhimu ya taifa, huku wakihimiza umuhimu wa kuwa na msimamo thabiti wa kulinda taifa, kudumisha amani na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali hao, Mzee Omary Suleiman, mfanyabiashara maarufu katika Soko la Kinondoni, alieleza kuwa vurugu zilizojitokeza hivi karibuni zilisababishwa na uchochezi wa makusudi. Alisisitiza kuwa ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kuwa matukio ya aina hiyo hayajirudii tena.
“Tanzania ni mimi, na mimi ni nchi. Tunaomba Watanzania wote waunge mkono jitihada hizi ili Tanzania ibaki salama, yenye amani na utulivu,” alisema Mzee Suleiman kwa msisitizo.
Tamko hilo limetolewa kufuatia ushirikiano wa karibu kati ya wajasiriamali na Taasisi ya MICIRA, taasisi inayojihusisha na utoaji wa elimu ya uraia kwa wafanyabiashara. Elimu hiyo imeelezwa kuwa chachu ya kuongeza uelewa kuhusu haki, wajibu na umuhimu wa kulinda amani ya taifa.
Katika mahojiano ya nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo walitoa maoni yao, akiwemo Husein Bambe, Kiongozi wa Wajasiriamali Ubungo; Bakari Sufia kutoka Ilala; na Pelagia Michael, Makamu Mwenyekiti wa Wajasiriamali Kinondoni. Kwa pamoja walisisitiza kuwa amani ni msingi wa biashara endelevu, maendeleo ya kijamii na ustawi wa Taifa la Tanzania.




