UTT AMIS KUSOGEZA HUDUMA ZA UWEKEZAJI KARIBU NA WANANCHI - MKUTANO MKUU WA MWAKA 2025
Na Nicolas Mushi, Dar es Salaam.
TAASISI ya Serikali ya uwekezaji wa pamoja(UTT AMIS) imeeleza kuwa mkakati wake mkubwa kwa sasa ni kusogeza huduma za uwekezaji karibu na wananchi kupitia teknolojia na upanuzi wa ofisi mikoani, ili kuwafikia Watanzania wengi ambao bado hawajanufaika na fursa za mifuko ya uwekezaji nchini.
Akizungumza leo Desemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Simon Migangala, amesema licha ya ongezeko la wawekezaji, bado idadi kubwa ya Watanzania haijafikiwa, jambo linaloifanya taasisi hiyo kuongeza jitihada za elimu na upatikanaji wa huduma.
“kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya simu na mfumo wa portal, sasa mwekezaji anaweza kuwekeza popote alipo bila kulazimika kufika ofisini, hatua inayolenga kuvunja vikwazo vya kijiografia na muda”,Amesema.
Ameongeza kuwa katika mwaka uliopita, UTT AMIS ilifungua ofisi mpya Morogoro na Kahama mkoani Shinyanga, kama sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi wa mikoa.
Aidha Kupitia maboresho hayo, Migangala amesema idadi ya wawekezaji wapya imeongezeka kwa kasi, ambapo zaidi ya wawekezaji 150,000 walijiunga ndani ya mwaka mmoja, na kufanya jumla ya wawekezaji kufikia zaidi ya laki tano.
Amesema ukuaji huo umechangiwa pia na kuimarika kwa mifuko ya uwekezaji, ikiwemo Mfuko wa Umoja uliofikia thamani ya zaidi ya Sh bilioni 400, huku baadhi ya mifuko ikipata faida inayozidi asilimia 15.
Migangala alieleza kuwa thamani ya mifuko yote ilisimama Sh trilioni 3.2 mwishoni mwa mwaka, kutoka Sh trilioni 2.2 mwaka uliotangulia, hatua inayodhihirisha imani ya wawekezaji na ufanisi wa mifumo ya taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS, Profesa Faustin Kamuzora, amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji.
Profesa Kamuzora amewataka waandishi wa habarikushirikiana na taasisi za fedha kutoa elimu kwa umma,huku akisisitiza kuwa uwekezaji katika masoko ya mitaji ni nyenzo muhimu ya kuinua kipato cha Mtanzania na kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050
![]() |
| Mwenyekiti w Bodi ya UTT AMIS Profesa Fausitin Kamuzola akizungumza na wadau WA UTT katika Ikumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. |
. 
