Waziri Kapinga Apongeza FCC kwa Jitihada Kubwa za Kulinda Walaji na Kudhibiti Bidhaa Feki
Na Hawa Ismail- Dar es salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ameipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa mchango wake mkubwa katika kudhibiti bidhaa feki, kulinda maslahi ya walaji, na kusimamia muunganiko wa makampuni makubwa ili kuhakikisha ushindani wa haki katika soko la biashara nchini.
Akizungumza leo Novemba 24, 2025 jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za FCC, Waziri Kapinga alisema kuwa ziara hiyo imelenga kuimarisha misingi ya utendaji kazi ili kuongeza ufanisi wa taasisi hiyo.
“Tunatambua kuwa Watanzania ndio walaji wetu wakuu, na kikao cha leo kinalenga kuboresha namna ya utendaji kazi ili kufikia matarajio yao. Pia tunatafuta njia bora zaidi za kuwafikia walaji na kupata mrejesho wa kazi zetu kwa urahisi,” alisema Mhe. Kapinga.
Aidha, Waziri Kapinga alisisitiza kuwa FCC imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha ubunifu na kuongeza ufanisi katika udhibiti wa bidhaa feki, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa walaji na soko la ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, Bi. Hadija Juma Ngasongwa, alieleza kuwa tume hiyo inaendelea kuratibu shughuli zake kwa kuzingatia falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kuwezesha taasisi za umma kutatua changamoto za wananchi, hususan katika sekta ya biashara.
Bi. Ngasongwa aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, FCC imekuwa ikichambua miamala ya muunganiko wa makampuni kwa lengo la kukuza mitaji na kuokoa ajira katika baadhi ya viwanda na kampuni zinazokumbwa na changamoto.
“Kuanzia Desemba 1, 2025, tumeanzisha zoezi la kurekodi usafirishaji wa bidhaa zote zinazoingia nchini. Hatua hii itasaidia kuzichunguza kwa kina na kudhibiti uingiaji wa bidhaa feki na zisizokidhi viwango,” alifafanua Bi. Ngasongwa.




