UVCCM Dar es Salaam: Wataka amani kupitia maridhiano
Na Hawa Ismail- Dar es salaam
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Mohamed Ramadhani, amesema kuwa matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yameacha maumivu makubwa kwa jumuiya ya vijana na taifa kwa ujumla. Ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza utamaduni wa amani na kuepuka vurugu, akisisitiza kuwa si hulka ya taifa la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24, 2025, jijini Dar es Salaam, Nasra alitoa pole kwa familia zote zilizoathirika na vurugu hizo, hasa waliopoteza wapendwa wao wakati wa na baada ya uchaguzi mkuu. Alisema ni muhimu taifa kujifunza kutokana na yaliyotokea na kujenga misingi ya maridhiano.
“Siasa ni ushindani wa hoja, na nguvu ya hoja ndiyo inayoshinda. Hata pale ambapo kuna kutokukubaliana, bado zipo njia nyingi za kutafuta suluhu. Maandamano yenye tija ni yale yanayozingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zilizopo,” alisema Nasra.
Aidha, alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ameshaunda Tume ya Uchunguzi kuchunguza matukio ya vurugu hizo. Tume hiyo inaongozwa na Mheshimiwa Jaji Othman Chande na inalenga kujenga maridhiano na kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za kitaifa.
Nasra alibainisha kuwa wajumbe wa Tume hiyo ni wastaafu wenye uzoefu mkubwa na hawana maslahi ya kisiasa, hivyo wanatekeleza jukumu lao kwa kutumia maarifa, busara na uzalendo. Alitoa mfano wa Profesa Ibrahim Juma, mmoja wa wajumbe wa Tume hiyo, ambaye aliwahi kuongoza Mahakama ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 20 na kushughulikia kesi mbalimbali, ikiwemo za vyama vya upinzani.
Vilevile, alitaja uwepo wa IGP Mstaafu Said Mwema katika Tume hiyo, akisema kuwa uzoefu wake wa zaidi ya muongo mmoja tangu astaafu unampa uwezo wa kutoa mchango mkubwa katika uchunguzi huo, hasa kwa kuzingatia uelewa wake wa mifumo ya utendaji wa Jeshi la Polisi.
Kwa ujumla, Nasra alisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na kuhimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani, haki na utulivu wa nchi.


