Breaking News

TAJU Yalaani Vurugu, Yataka Watanzania Kudumisha Amani na Uzalendo

Na Hawa Ismail-Dar es Salaam 

Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali Tanzania Jumuishi (TAJU), Ndonge Said Ndonge, amelaani vikali vitendo vya vurugu vilivyosababisha uvunjifu wa amani, hasa kwa watu wenye ulemavu, na hata wengine kupoteza maisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ndonge alisisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi na kuvitaka vyama vya siasa pamoja na viongozi wa dini kutumia nafasi zao kwa busara ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye utulivu na mshikamano.

 “Zao la amani ni haki muhimu kwa dunia ya sasa. Ili kulinda amani yetu, hatupaswi kuiga mataifa mengine yanayokumbwa na vurugu zisizo na suluhu. TAJU inawaasa Watanzania kuacha kuiga mambo ya nje yasiyo na manufaa kwa taifa letu,” alisema Ndonge.

Aidha, alihimiza Watanzania kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya, akisisitiza kuwa si kila kinachochapishwa mtandaoni kinafaa kuigwa.

Ndonge pia alizungumzia dhana ya uzalendo wa kweli, akisema kila Mtanzania anapaswa kujitathmini kwa kuzingatia namna anavyolinda na kulipenda taifa lake.

 “Mzalendo wa kweli si mbinafsi; hutanguliza maslahi ya taifa kabla ya yake binafsi. Tunapaswa kuiga mfano wa viongozi wetu waasisi kama Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Abeid Amani Karume na Edward Moringe Sokoine, waliopigania taifa kwa moyo wa uzalendo wa dhati,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu wa TAJU, Innocent Gabriel Siriwa, alitoa wito kwa Watanzania wote kufuata taratibu za kisheria wanapokuwa na malalamiko au kutoridhika na jambo fulani, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kusababisha vurugu.

 “Tufuate taratibu za kisheria ili maoni yetu yasikike na yafanyiwe kazi. Vurugu hazileti suluhu bali zinadidimiza maendeleo,” alisema Siriwa.

TAJU imeitaka serikali na Watanzania kwa ujumla kusameheana kwa yote yaliyotokea, ikisisitiza kuwa msamaha ndio msingi wa maridhiano na amani ya kweli.

 “Popote tulipo, tuendelee kuitunza, kuilinda na kuendeleza amani ya taifa letu la Tanzania,” alihitimisha Ndonge.