NLD Yafunga Kampeni Handeni; Doyo Asema Serikali Yake Itakuwa ya Uwajibikaji, Uwazi na Ufanisi, Asema Sera za NLD Zinatokana na Utafiti wa Kina na Zina Mwongozo wa Kitaalamu
Handeni, Tanga
Chama cha NLD leo kimefunga rasmi kampeni zake za urais katika mkutano mkubwa uliofanyika Misima, wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika mkutano huo, Mgombea Urais wa NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amesema endapo wananchi watamchagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali yake itakuwa serikali jumuishi, yenye uwajibikaji, uwazi na ufanisi, itakayoweka wananchi kwanza katika kila hatua ya maamuzi.
Mhe. Doyo amesema serikali yake itaanza kwa kupunguza matumizi yasiyo na tija ili kuhakikisha kila shilingi ya umma inaleta matokeo chanya kwa wananchi.
“Serikali yangu itakuwa ya mfano. Nitaanza mimi mwenyewe kwa kuonyesha nidhamu ya matumizi na uwazi wa fedha za umma. Tutapunguza gharama zisizo na maana ambazo zimekuwa mzigo kwa wananchi,” alisema Mhe. Doyo.
Amebainisha pia kuwa hana tatizo na wagombea wengine wanaonukuu au kutumia baadhi ya sera zake, akisisitiza kuwa sera za NLD zinatokana na utafiti wa zaidi ya miaka mitatu kupitia Ilani ya Chama inayobebwa “Tunu ya Uzalendo, Haki na Maendeleo.”
“Sera zetu si za kubuni leo kwa ajili ya kampeni. Zimetokana na utafiti wa kina unaoangalia maisha halisi ya Mtanzania. Wapo wanaoiga, lakini tofauti ni kwamba sisi tumeziasisi na tumezipanga kitaalamu ndani ya Ilani yetu,” alifafanua Mhe. Doyo.
Akizungumzia sera ya afya, Mhe. Doyo alisema kuwa serikali ya NLD itahakikisha marehemu wote wanasamehewa gharama za matibabu pindi umauti unapomkuta mgonjwa hospitalini. Amesema hatua hiyo inalenga kutoa heshima kwa walipa kodi wema ambao wamechangia maendeleo ya taifa wakati wa uhai wao.
“Iwapo marehemu alikuwa mlipa kodi mzuri, gharama za matibabu yake zitatumika kama ubani au sanda kwa heshima ya mwisho. Hii ni sera ya kibinadamu, na ipo wazi katika sura ya nane ya Ilani ya NLD,” alisema Mhe. Doyo.
Ameongeza kuwa baadhi ya wagombea wengine wanaahidi sera ambazo hazitekelezeki kwa kuwa hazina mwongozo wa kitaalamu katika ilani zao, tofauti na NLD ambayo imeweka mikakati thabiti ya utekelezaji.
“Nimejiandaa kwa miaka mingi, sijakurupuka. Nichagueni niwe Rais niwatumikie kwa moyo wa uzalendo na kwa misingi ya haki na maendeleo,” alihitimisha Mhe. Doyo.
Aidha, Meneja wa Kampeni wa Mgombea Urais huyo, Ndugu Pogora Ibrahim Pogora, aliwaomba Watanzania kumpa kura Mhe. Doyo, akisisitiza kwamba taifa linahitaji kiongozi atakayeendesha serikali kwa tija na kwa maslahi ya wananchi kama waajiri, si mtawala.
“Mhe. Doyo ni mtu msikivu, mwenye nia njema na anayeshaurika. Wana Handeni, Tanga na Watanzania kwa ujumla, mabadiliko ya kweli yapo chini ya mpambanaji huyu. Yeye ndiye mtu sahihi wa kuifanya Tanzania ifikie uchumi unaogusa maisha ya kila siku ya wananchi,” alisema Pogora.
Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchambuzi wa NLD, Mhe. Don Waziri Mnyamani, alisema chama hicho kimejipanga kikamilifu kwa uchaguzi wa mwaka huu, na ndiyo maana kimeweza kusimamisha wagombea mbalimbali kote nchini
“Tumeweza kufika zaidi ya mikoa 28 na wilaya 80. Tupo tayari kwa uchaguzi huu kwa sababu tumejikita kwenye sera madhubuti zinazotokana na ilani bora yenye malengo thabiti ya Watanzania,” alisema Mnyamani.
Mwisho wa mkutano huo, Mhe. Doyo aliwashukuru wananchi wa Tanga, Handeni na Watanzania kwa ujumla kwa mapokezi makubwa na ushirikiano waliouonesha tangu mwanzo wa kampeni, akiwataka waendelee kudumisha amani, umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu.


