DC Maiga Azindua Mahema ya Biashara kwa Vijana na Wanawake Mpaka wa Mutukula
Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Mhe. Hamisi Mayamba Maiga, amezindua rasmi mahema maalumu ya biashara katika mpaka wa Mutukula, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya biashara kwa vijana na wanawake. Mradi huo unatekelezwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Wakulima na Viwanda Tanzania (TCCIA) kwa kushirikiana na Taasisi ya AGRA, ukiwa na lengo la kukuza biashara za mpakani na kuongeza usalama wa shughuli za kiuchumi.
Uzinduzi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi unaolenga mikoa ya mipakani, ambapo awali ulitekelezwa Kigoma na sasa umefika Kagera.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Maiga aliipongeza TCCIA na AGRA kwa juhudi zao za kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, hasa vijana wanaojihusisha na biashara za mazao, mboga mboga na matunda katika maeneo ya mipakani.
“Nawapongeza sana TCCIA na AGRA kwa kuandaa na kutekeleza mradi huu kwa viwango vya juu. Hii ni fursa adhimu kwa vijana wetu, hasa walioko maeneo ya mpakani,” alisema Maiga.
“Serikali inaunga mkono jitihada hizi. Endeleeni kuzifikisha katika mipaka yote nchini.”
Aidha, aliwataka vijana na wafanyabiashara kutumia mahema hayo kama majukwaa ya kupata taarifa za masoko, kuripoti changamoto zisizo za kikodi, na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
“Tumieni jukwaa hili kutafuta taarifa, kutangaza bidhaa zenu, na kuripoti vitendo kandamizi ili mfanye biashara kwa ufanisi na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” aliongeza.
Uzinduzi huo uliambatana na mafunzo ya _Whistle Blowing_ kwa wafanyabiashara wa Mutukula, yaliyolenga kupambana na vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs), kuripoti changamoto kwa njia za kidijitali, kuboresha ubora wa bidhaa, na kutumia mitandao ya kijamii kupanua masoko.Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCCIA mkoa wa Kagera, Bw. Rwechungura Mali, alisema chemba hiyo itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupitia mafunzo na kuwaunganisha na mitandao ya kibiashara. Aliwahimiza wafanyabiashara kujiunga na TCCIA ili kufungua fursa zaidi za ukuaji.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara mpakani, kuimarisha usalama wa bidhaa, kupunguza rushwa na gharama za uendeshaji, pamoja na kukuza uchumi wa vijana na wanawake. Tayari utekelezaji wake katika mikoa ya Kigoma na Kagera umeanza kuonyesha mafanikio chanya.


