Breaking News

DC ITUNDA AMWAKILISHA RC MBEYA MAHAFALI YA CHUO CHA MAGEREZA RUANDA






Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, katika mahafali ya Chuo cha Magereza Ruanda kilichopo jijini Mbeya.

Katika hafla hiyo, Mhe. Itunda alitoa vyeti kwa wahitimu zaidi ya 260 wa mafunzo ya ufundi stadi ya fani mbalimbali. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Itunda alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kugharamia mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kujiajiri, pamoja na kuimarisha miundombinu ya elimu nchini.

Amesema juhudi hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuinua sekta ya elimu na ajira.

Aidha, alimshukuru Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya kwa maandalizi mazuri ya hafla hiyo, pamoja na uongozi wa chuo kwa jitihada za kutoa elimu bora inayowaandaa wahitimu kukabiliana na changamoto za maisha.

Mhe. Itunda aliwahimiza wahitimu kutumia vyema ujuzi walioupata kama chanzo cha kujiletea maendeleo na kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, nidhamu, na uzalendo katika maeneo yao.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa zoezi la ugawaji wa vyeti kwa wahitimu wote 260 ambapo wadau wa elimu, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wazazi na walezi walihudhuria na kushuhudia tukio hilo muhimu


.