Tiba Shufaa Yatajwa Kama Mkombozi kwa Wagonjwa wa Maradhi wenye maumivu Sugu – Wizara ya Afya Yatoa Wito kwa Jamii na Wadau
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba Shufaa, Wazee na Utengamao kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Mwinyikondo Amiri, amesema tiba shufaa ni huduma jumuishi inayojumuisha hatua zote muhimu za afya kuanzia ugunduzi wa ugonjwa, matibabu, hadi muendelezo wa huduma ikiwemo utengamao kwa wagonjwa wenye maradhi sugu.
Akizungumza leo Oktoba 11, 2025 jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya wagonjwa wenye maradhi ya kudumu, Dkt. Amiri alieleza kuwa lengo kuu ni kuboresha ubora wa huduma kwa wagonjwa wanaoathiriwa na magonjwa ya muda mrefu.
“Huduma za tiba shufaa nchini Tanzania zilianza mwaka 1996 kupitia Taasisi ya Ocean Road, ambapo wagonjwa wa saratani walikuwa wa kwanza kunufaika. Baadaye huduma hizi ziliwafikia wagonjwa wa VVU, matatizo ya moyo na damu,” alisema Dkt. Amiri.
Aliongeza kuwa tiba shufaa inalenga kuondoa maumivu sugu na ya kudumu kwa kutumia dawa maalum, ikiwemo dawa ya mofia ya maji, ambayo hutolewa kwa wagonjwa wenye maumivu makali hasa wa saratani. Alisisitiza kuwa upatikanaji wa dawa hiyo katika Taasisi ya Ocean Road umefikia asilimia 100.
Dkt. Amiri pia alieleza kuwa huduma hizi zinatolewa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kidini na binafsi. Alizitaja taasisi za KKT mkoani Arusha, vituo maalum mkoani Tanga, taasisi ya PASADA ya Kanisa Katoliki jijini Dar es Salaam, pamoja na CCP Medicine kama washirika muhimu katika utoaji wa huduma hizo.
Pamoja na mafanikio hayo, alibainisha kuwa changamoto kubwa inayokabili huduma za tiba shufaa ni ukosefu wa elimu na uelewa miongoni mwa wananchi, ambapo asilimia kubwa hawajui umuhimu wa huduma hizo.
“Tiba shufaa inalenga kuondoa maumivu ya kimwili, kisaikolojia, na kijamii kwa mgonjwa na familia inayomhudumia,” alisisitiza Dkt. Mwinyikondo.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa madaktari, wauguzi, wafamasia, wanasaikolojia, pamoja na viongozi wa dini na kiroho kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za tiba shufaa. Alisema lengo kuu ni kumhudumia mgonjwa hadi mwisho wa maisha yake kwa heshima, huruma na uelewa mpana kutoka kwa familia na jamii.






