CUF Yalilia Uharibifu wa Mabango Mbagala, Viongozi Watoa Ahadi za Mageuzi ya Kiuchumi na Kijamii
Katibu wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Bakonzi, ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuhakikisha ulinzi wa mabango ya kampeni ya chama hicho baada ya mabango mawili yaliyowekwa maeneo ya Mbagala Mission na Mbagala Sabasaba kuchanwa na watu wasiojulikana.
“Tumeathirika na uharibifu wa mabango yetu. Tayari tumeandaa mabango mengine kuyachukua nafasi ya yaliyoharibiwa. Hata hivyo, tukikumbana tena na vitendo hivi, tutachukua hatua za kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaohusika,” alisema Bakonzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amewataka Watanzania kupambana na maadui wakuu watatu wa maendeleo: ujinga, maradhi na umaskini. Alisema matatizo haya yanachangiwa na sera zisizolenga maendeleo ya wananchi, licha ya Tanzania kuwa nchi tajiri yenye rasilimali nyingi.
“Tuna ardhi yenye rutuba, mazao kama alizeti, ufuta na karanga. Hatupaswi kuwa maskini. Tanzania ni ya pili Afrika kwa idadi ya ng’ombe, lakini hatuna viwanda vya kuchakata nyama. Hili ni eneo muhimu la uwekezaji kwa ajili ya ajira kwa vijana wetu,” alieleza Prof. Lipumba.
Aliongeza kuwa iwapo CUF itapewa nafasi ya kuongoza, watahakikisha miundombinu ya maeneo kama Kiburugwa inaboreshwa. Pia alisisitiza kuwa Tanzania ikiwa ni nchi ya tatu kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika, ina uwezo wa kutengeneza malighafi kwa ajili ya betri za magari ya umeme, hatua itakayoiweka nchi katika mstari wa mbele wa mapinduzi ya kiteknolojia.
Katika sekta ya afya, Prof. Lipumba alisisitiza umuhimu wa lishe bora kwa watoto na wajawazito, akisema:
“Tuwekeze kwenye afya. Yote yanawezekana tukipata serikali inayojali na katiba imara inayowajibika kwa wananchi.”
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia CUF, Shekh Said Kinyogoli, aliahidi kuwa endapo atachaguliwa, atawatumikia wananchi kwa uzalendo. Aliahidi kupinga unyanyasaji wa wananchi wanaouziwa mali zao kwa sababu ya mikopo na kusimamia kwa karibu huduma Hospitali ya Mbagala ili ziwe bora na zisizo na ubaguzi.
Naye mgombea udiwani wa Kata ya Kiburugwa, Omary Said Mkingie, aliahidi kuboresha miundombinu ya barabara, kurejesha mifereji ya maji na kuleta maendeleo ya kweli katika kata hiyo.
