PASS Trust Business Forum Yachochea Uwekezaji wa Kilimo na Ushirikiano wa Taasisi za Fedha Nchini
Katika kilele cha maadhimisho ya miaka 25 PASS Trust Business Forum yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PASS Trust na Mkurugenzi wa Biashara, Adam Kamanda, ameeleza kuwa taasisi hiyo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Denmark, ikiwa na lengo la kuchochea kilimo biashara, ufugaji, uhifadhi wa misitu na kuongeza uwekezaji kupitia taasisi za kifedha.
Kamanda alibainisha kuwa kongamano hilo limeunganisha mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar, likiwaleta pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za fedha nchini. Alisema, “Tumefanikisha kuwaleta wadau wote wa sekta ya kilimo kutoka mikoa ya Njombe, Arusha, Kahama, Moshi na Bukoba ili kujadili fursa na changamoto zinazowakabili.”
Kwa mujibu wa Kamanda, PASS Trust Forum imeweza kutoa dhamana ya takribani shilingi trilioni 2.4 mwaka huu pekee. Aidha, alieleza kuwa kupitia uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imeongeza uwekezaji wa shilingi trilioni 1.2 katika sekta ya kilimo, hususan kwenye bajeti ya kilimo cha umwagiliaji.
Hadija Seif, Meneja Mahusiano kutoka Benki ya Washirika makao makuu Dodoma, alieleza kuwa ushirikiano wao na PASS Trust umeleta mafanikio makubwa kwa wakulima. “Tuna zaidi ya potifolio ya bilioni nane chini ya PASS, na wamekuwa msaada mkubwa kwa wakulima nchini,” alisema Hadija. Hata hivyo, alitaja changamoto za masoko, pembejeo na elimu ya kilimo kama vikwazo vinavyohitaji kushughulikiwa kwa haraka.
Kwa upande wake, Daniel Sumpo kutoka Equity Bank, alieleza kuwa wakulima wadogo wanakabiliwa na ugumu wa kupata mikopo. Kupitia PASS Trust Business Forum, benki hiyo imekuwa ikitoa garantii kwa wakulima ili waweze kupata mitaji na nyenzo bora za kilimo, hivyo kuongeza tija katika uzalishaji.
Maadhimisho haya yameonesha dhamira ya dhati ya PASS Trust Business Forum katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia ushirikiano wa taasisi za fedha, serikali na wadau wa maendeleo. Kwa kuwepo kwa mazingira wezeshi na bajeti madhubuti, Tanzania ina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wake kupitia kilimo endelevu.



