Mkuu wa Wilaya ya Ilala na Riziki Lulida waongoza Maombi Maalumu ya Watu Wenye Ulemavu kuelekea Uchaguzi Mkuu
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogoro, ameshiriki katika kongamano la watu wenye ulemavu lililofanyika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya maombi maalumu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Oktoba 25, 2025, Mhe. Mpogoro aliishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia kwa ufanisi mchakato wa maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo utoaji wa taarifa kwa kila hatua muhimu.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi. Kwa niaba ya Serikali, nawahakikishia kuwa Dar es Salaam ni salama na Ilala ni salama sana. Tunao wajibu kama Serikali kusimamia amani na usalama wa Watanzania,” alisema Mpogoro.
Mhe. Mpogoro alitoa wito kwa wananchi kutupilia mbali maneno ya uchochezi yanayosambazwa mitandaoni, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na mshikamano. Alieleza kuwa licha ya tofauti za vyama, makabila na rangi, Watanzania wameendelea kushikamana kwa dhati.
Aidha, alisifu uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wananchi wote kujitafutia riziki kupitia kazi mbalimbali. Alisisitiza umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani, akiwahakikishia wananchi ulinzi na usalama nchi nzima.
Kwa upande wake, Mhe. Riziki Lulida, Mbunge Mstaafu wa kuteuliwa na Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Riziki Lulida, alisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo nchini Tanzania.
“Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kwa watu wenye ulemavu. Wenye ulemavu wa usikivu mdogo wanachimba dhahabu, na wengine wanapanda miti ili kusaidia mabadiliko ya tabianchi. Tanzania inaelekea kuwa nchi ya kijani,” alisema Lulida.
Sheikh Mohamed Abdallah, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Tanzania (JMAT), alihitimisha kwa kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kuharibu au kuzuia amani ya nchi.


