Breaking News

KINYOGOLI ANGURUMA MBAGALA KIJICHI AAHIDI KUSIMAMIA ELIMU BURE KUONDOA MICHANGO MASHULENI

 

Katika kampeni za hadhara zilizofanyika Oktoba 26, 2025 katika eneo la Kijichi, wagombea wa ubunge kupitia Chama cha Wananchi CUF wameeleza kwa kina mikakati yao ya kuleta mabadiliko katika maeneo ya Mbagala, Kigamboni na Temeke endapo watapata ridhaa ya wananchi.

Mgombea wa ubunge wa jimbo la Mbagala, Sheikh Said Juma Kinyogoli, aliahidi kusimamia elimu bure katika shule ya Kijichi na kuboresha huduma za afya. Alieleza kuwa vijana wa bodaboda watapatiwa mafunzo ya udereva na leseni rasmi, hatua ambayo inalenga kupunguza hasira na changamoto zinazowakumba vijana wa Mbagala.

“Nitahakikisha kwenye hospitali zote za serikali hakuna malipo ya kumuona daktari katika miezi sita ya mwanzo endapo nitachaguliwa,” alisema Kinyogoli.

Mgombea wa ubunge wa Kigamboni kupitiaChamaChaWananchiCUF , Wakili Msomi, alisisitiza umuhimu wa amani na haki ya kupiga kura. Alieleza kuwa Oktoba 29, 2025 ni siku ya kutimiza wajibu wa kidemokrasia bila maandamano au vurugu.

 “Kazi itakuwa moja tu – ni kwenda kupiga kura na siyo vurugu,” alisisitiza.

Mgombea wa ubunge wa Temeke, Zainabu Mndolwa Amiri, alieleza kuwa siasa ni sehemu ya maisha na kupiga kura ni njia ya kutetea haki. Alionyesha imani yake kwa Jeshi la Polisi la Tanzania katika kulinda usalama wa wananchi wakati wa uchaguzi.

Meneja wa kampeni wa CUF, Rajab, alieleza kuwa chama hicho kitasimamia elimu, ajira kwa vijana na marekebisho ya katiba endapo kitapata nafasi ya kuongoza.

“Hatutishiki na maneno ya mambe kimanbi. Wananchi wataenda kupiga kura kwa ulinzi na usalama wa kutosha,” alisema.

Diwani wa kata ya Kijichi, Haji Mohamed Mgaya, aliahidi kusimamia miradi ya TASAF, maji safi, miundombinu na mifereji ili kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.