CCM Temeke Yatoa Wito wa Kudumisha Amani na Ushiriki Mkubwa Katika Uchaguzi
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke kimewataka Watanzania kuwapuuza watu wenye nia ya kuvuruga amani ya taifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Badala yake, wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura litakalofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Daniel Sayi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anatarajiwa kufanya ziara wilayani humo tarehe 23 Oktoba, 2025.
"Kwa hivi karibuni, kuna baadhi ya watu wenye nia ovu ya kuchochea vurugu, hasa kipindi hiki cha uchaguzi. Tunawaomba watu wa Temeke wawapuuze na wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu," alisema Sayi.
Aidha, Sayi alieleza kuwa CCM inajivunia mafanikio ya utekelezaji wa ilani yake, hususan katika sekta ya afya, ambapo Hospitali ya Temeke imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa, hatua iliyosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Zena Yussuf Mgaya, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika tarehe 23 Oktoba, kwa ajili ya kumsikiliza Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tunawaomba mjitokeze kwa wingi kuja kumsikiliza mgombea wa urais, tujue nini ametuandalia. Mkutano huo utakuwa na jukumu la kunadi sera pamoja na kuwanadi wagombea wa ubunge," alisema Mgaya.
