Wilson Elias Aahidi Mageuzi Makubwa: Maji Safi, Reli ya Abiria na Utalii wa Baharini Kawe
Na Hawa Ismail, Dar es Salaam
Mgombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha _Alliance for Democratic Change (ADC)_, Wilson Elias, ameahidi kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo endapo atachaguliwa kuwa Rais. Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika kampeni zake zilizofanyika jimboni Kawe, Elias alieleza dhamira yake ya kufunga mtambo wa kuchakata maji ya bahari ili yawe safi na salama kwa matumizi ya nyumbani. Mtambo huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la bahari lililopo Kawe.
Katika sekta ya miundombinu, Elias alitangaza mpango wa kujenga reli ya abiria jijini Dar es Salaam, akisema kuwa treni hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 1,000 kwa wakati mmoja. “Kawe mpaka Mbagala kutakuwa na treni la abiria ambalo litabeba wananchi zaidi ya elfu 1000 kwa wakati mmoja. Hivyo kuwepo kwa treni ndio suluhisho la usafiri katika jiji la Dar es Salaam,” alisema Elias.
Akigusia masuala ya haki za binadamu, mgombea huyo aliahidi kulipa kipaumbele kwa wanasheria kufanya kazi kwa haki na usawa bila upendeleo kwa watu wenye uwezo wa kifedha. Alisisitiza kuwa wanasheria wanapaswa kuwatetea watu wanyonge kama vile wanawake, watoto yatima na wale wasiokuwa na sauti katika jamii.
Katika kukuza uchumi wa Kawe, Elias alieleza nia yake ya kuifanya Kawe kuwa kitovu cha utalii wa baharini. Alisema kuwa fukwe za Kawe zitatumika kama fursa ya kiuchumi kwa biashara na utalii. “Juzi nilikuwa Forodhani Zanzibar, wenzetu wanabahari kama hii unayoiyona wanafanya biashara hadi saa sita za usiku. Hivyo tutatumia fukwe zetu kwa ajili ya kutengeneza pesa,” aliongeza.
Chama cha _Alliance for Democratic Change (ADC)_ kimefanikiwa kuweka wagombea kuanzia nafasi ya urais hadi madiwani, kikilenga kuleta mabadiliko ya kweli katika uongozi wa taifa.




