Breaking News

Viongozi wa Dini Washiriki Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani kwa Kuliombea Taifa la Tanzania*

 


Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani kwa Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika kwa mafanikio makubwa mnamo tarehe 20 Septemba 2025, katika viwanja vya Mnazi Mmoja (Mashujaa wa Uhuru). Tukio hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa viongozi wa dini mbalimbali, likiwa na lengo kuu la kuliombea Taifa la Tanzania ili kuendeleza na kudumisha amani iliyopo.





Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh Walid Omari Kawambwa, alisisitiza kuwa amani ni msingi wa kila jambo. “Bila amani hakuna shughuli yoyote inayoweza kufanyika—iwe ya kidini, kisiasa au kijamii. Amani ni msingi wa maendeleo na mshikamano,” alisema Sheikh Kawambwa.


Katika hotuba yake, Sheikh Kawambwa alitoa wito kwa wananchi wote, hususan wakazi wa Dar es Salaam, kuilinda amani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi. Alionya kuhusu viashiria vya baadhi ya watu wenye nia mbaya wanaotaka kuleta machafuko nchini. “Sisi kama viongozi wa dini—mashehe na maaskofu—tumeungana na tunamtangazia ulimwengu kuwa hatutakubali Taifa letu kuingia katika machafuko. Tutamwelekea Mwenyezi Mungu kwa maombi, tukiwaombea wenye nia mbovu waachane na mipango yao,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mchungaji Paul Bendera alitoa tahadhari dhidi ya kupoteza amani kwa kusikiliza maneno ya watu wasio na nia njema. “Tusilazimishe kupoteza amani tuliyo nayo. Sisi kama viongozi wa dini hatutamani kuona migongano baina ya serikali, viongozi na wananchi. Tanzania ni nchi ya amani, na ni wajibu wetu sote kuilinda,” alisema Mchungaji Bendera.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa _“Amani Yetu, Fahari Yetu. Tuna Yetu.”_ Ujumbe huu ulisisitiza kuwa kila Mtanzania ana jukumu la kuilinda na kuendeleza amani ya taifa.