Breaking News

Mawakili Vijana na wadau washiriki kongamano la kisheria ili kusimamia haki, demokrasia na sheria kwa njia ya kidigitali kuelekea uchaguzi mkuu 2025

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

*📍Dar es Salaam, Septemba 19, 2025*

Katika kongamano la kila mwaka la Umoja wa Mawakili Vijana (AYL) chini ya Tanganyika Law Society (TLS), viongozi na wataalamu wa sheria wameangazia nafasi ya mawakili vijana katika kuimarisha matumizi ya teknolojia, utawala bora na haki katika muktadha wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Wakili Ukashu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa AYL-TLS, alieleza kuwa kongamano hilo limewaleta pamoja wataalamu kutoka sekta mbalimbali ili kufafanua mada zinazolenga kuhamasisha na kuwawezesha mawakili vijana kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kidigitali yanayoathiri demokrasia.

“Watu wengi siku hizi hawakutani ana kwa ana, bali kupitia mitandao. Tunatafuta namna ya kutumia utetezi wa kidemokrasia kupitia njia za kidigitali,” alisema Wakili Ukashu.

Kwa upande wake, Wakili Fatma Songoro, mtaalamu wa sheria za teknolojia, alisisitiza kuwa mawakili vijana wana jukumu la kusimamia sheria zinazoongoza matumizi ya teknolojia katika mifumo ya kidemokrasia.

“Tumejifunza mengi leo. Tunapaswa kuhakikisha mifumo ya kidigitali inaheshimu haki za binadamu na inatoa fursa kwa wananchi kushiriki bila vikwazo,” alieleza Songoro.

Hata hivyo, Wakili Songoro alionya kuhusu changamoto ya usambazaji wa taarifa potofu mtandaoni, hasa katika kipindi cha uchaguzi, akisema:

“Kuna ‘misinformation na disinformation’—taarifa zisizo sahihi zinazolenga kuchafua majina ya watu kisiasa.”

Kongamano hilo, lenye kaulimbiu _“Safari ya Kidemokrasia, Kidigitali na Sheria”_, limeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa mawakili vijana kujadili na kuchangia mwelekeo wa taifa katika matumizi ya teknolojia kwa ajili ya haki na utawala bora.