Breaking News

Shekhe Mwaipopo Atoa Rai kudumisha Amani kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025



📍Dar es Salaam, Septemba 14, 2025*

Shekhe Mwaipopo amejitokeza hadharani kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini na kutoa wito kwa Watanzania, hususan wale wanaojiita wanaharakati, kuacha mara moja tabia ya kubeza na kutukana juhudi za Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ametahadharisha kuwa uchochezi wa aina hiyo unaweza kuhatarisha amani ya taifa, ambayo ni tunu isiyopaswa kuchezewa, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Akizungumza akiwa ofisini kwake Magomeni (Kagera), jijini Dar es Salaam, Shekhe Mwaipopo aliambatana na kundi la watu waliotambulika kama wazalendo na wapenda amani, ambao walisema kuwa mlengo wao ni mafanikio ya taifa na si siasa za vyama. Wakiwa na nia njema kwa serikali ya Rais Samia, walisisitiza umuhimu wa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.


Katika maelezo yake, Shekhe Mwaipopo alieleza kusikitishwa na kauli za baadhi ya watu mitandaoni, akiwemo Mange Kimambi, akisema:

“Tunashangaa kuona wakina Polepole na Mange Kimambi wanamtukana Rais. Wewe Mange hatukuelewi kabisa. Sisi kwa pamoja tunasema Samia atachaguliwa na atapita kwa kishindo.” alisema Mwaipopo 

Aliendelea kwa kuorodhesha mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa na Dkt. Samia, akihusisha miradi ya miundombinu, elimu, afya, na sera ya siasa za maridhiano ambayo imefungua milango kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara. Hata hivyo, alionya kuwa baadhi ya matokeo ya sera hizo hayakuwa mazuri, akitaja mienendo ya Tundu Lissu kama mfano.

Shekhe Mwaipopo pia alitoa wito kwa wanaharakati wote wenye mitazamo tofauti na Rais Samia, kuacha mara moja kumtukana kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa amani ya taifa ni muhimu kuliko tofauti za kisiasa.

Kwa pamoja, kundi hilo la wazalendo lilimwombea dua ya kheri Rais Samia kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, wakihimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kumpigia kura kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimemteua kuwania urais kwa mara nyingine.