Kikosi cha Polisi Wanamaji Wazindua Mpango wa Kuwawezesha Wasichana Kitaifa Kupitia Elimu ya Uokoaji Majini
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Kikosi cha Polisi Wanamaji jijini Dar es Salaam kimezindua mpango kabambe wa kutoa elimu ya uokoaji majini kwa wasichana kote nchini, kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi vyuo vikuu. Lengo kuu ni kuongeza ushiriki wa mabinti katika masuala ya usalama wa majini na kuimarisha uelewa wao kuhusu shughuli za ulinzi zinazofanyika baharini.
Akizungumza katika tukio hilo, Afisa wa Polisi ASP Anna Nicholaus Ugomba alisema kuwa mpango huo unalenga kufungua fikra za mabinti wadogo kuhusu umuhimu wa usalama wa majini na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika vikosi vya ulinzi. “Tunataka wasichana waelewe kinachofanyika ndani ya bahari, hasa kazi za vyombo vinavyolinda usalama wa maji,” alisema ASP Ugomba.
ASP Ugomba aliongeza kuwa elimu hiyo itasaidia kuvutia mabinti wengi kujiunga na kikosi cha wanamaji, hatua itakayochangia kwa kiasi kikubwa kupambana na uhalifu unaofanyika baharini. Alifafanua kuwa vigezo vya kujiunga na kikosi hicho ni pamoja na kuwa Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18, elimu ya angalau kidato cha nne hadi chuo kikuu, na afya njema.
Kwa upande wake, Benedictor Cherono alieleza kuwa mradi huo unalenga kuwahamasisha wasichana kutumia vipaji vyao na kujiunga na vikosi vya maji. “Tumefurahia kuona wadau wakileta wanafunzi kujifunza kwa kuuliza maswali. Tunaamini tumewajengea msingi wa maarifa ambao utawasaidia hata wakirudi shuleni,” alisema Cherono.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Diamond, Amanyisye Innocent, alieleza furaha yake baada ya kushiriki mafunzo hayo, akisema amejifunza kuhusu mbinu za uokoaji majini na sheria zinazohusiana na usalama wa maji kupitia kikosi cha polisi wanamaji kwa ushirikiano na UNODC
Naye ACP Shabani Mwananengule alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kushirikiana na jamii, na kwamba vyombo vya habari vitatumika kutoa elimu zaidi ili kuwahamasisha mabinti kujiunga na kikosi cha polisi wanamaji.


