Breaking News

MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KILOSA ACT WAZALENDO HASSAN MBARUKU AAHIDI KUMALIZA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kilosa mkoani Morogoro kupitia Chama cha ACT Wazalendo Hassan Thabiti Mbaruku ameahidi kumalizi migogoro ya wakulima na wafugaji endapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Mbaruku amebainisha hayo leo Septemba 22, 2025 akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa Ilani ya Chama kwa mwaka 2025 hadi 2026 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mgombea huyo kijana mwenye matamanio makubwa ya kuleta mageuzi na mapinduzi makubwa katika Jimbo hilo la Kilosa, ameeleza kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji ni moja ya changamoto sugu inayowakabili wananchi jimboni humo.

"Jimbo la Kilosa limekuwa na changamoto nyingi, lakini Ilani yetu ya Chama ya 2025/2026 imeelezea vizuri changamoto hizi na kama tukiifanyika kazi tutazitatua," amesema Mbaruku na kuongeza,

"Moja ya changamoto inayowakabili wananchi wa Kilosa ni migogoro ya wakulima na wafugaji, hii imekuwa ni changamoto kubwa ambayo imekuwa ikichangia wakulima kutoendelea,".

Hivyo Mbaruku amebainisha kuwa katika kumaliza migogoro hiyo, kama atachaguliwa atahakikisha anaishauri Serikali kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wakulima ili kufanya shughuli zao za kilimo, sambamba na kutenga maeneo maalum ya wafugaji na kuhakikisha hawaingiliani kwa maslahi ya kila upande.

Kwamba atahakikisha kunatengwa eneo la nyasi kwa ajili ya malisho ya mifugo ya wafugaji na kwamba njia hiyo anaamini italeta suluhisho la kudumu ya migogoro hiyo ya wakulima na wafugaji.

Kadhalika Mbaruku amesema endapo atachaguliwa amejipanga kutatua changamoto nyingine kama vile za afya kwa kuhakikisha anaboresha huduma za Hospitali ya Wilaya ya Kilosa pamoja na kuhakikisha Zahanati za Kata zinapandishwa hadhi ya kuwa Vituo vya Afya.

Kwamba changamoto nyingine atakazoshughulikia ni tatizo la ajira kwa vijana ambapo atahakikisha viaanzishwa viwanda vitakavyozalisha ajira, sambamba na kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao ya wana Kilosa.

Ameongeza kuwa atasimamia miradi ya barabara za mitaa na ujenzi wa mifereji ya maji kwani miundombinu hiyo kwa sasa sio mizuri, pamoja na hayo atahakikisha anafanya maboresho katika Sekta ya Elimu na kuondoa michango isiyo na tija kwa Shule za Msingi na Sekondari.