Kamishna Murilo: SSH 2530 Sio Namba Rasmi za Usajili
Na: Kelvin Kijo
Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, C.P Murilo, leo tarehe 04 Septemba 2025 jijini Dar es Salaam amezungumza na waandishi wa habari katika kituo kikuu cha polisi cha jijini, ambapo ametoa taarifa ya hali ya usalama na mafanikio ya jeshi hilo katika kipindi cha hivi karibuni.
Murilo amesema kuwa kati ya tarehe 16 hadi 25 Agosti 2025, jeshi la polisi liliendesha msako wa kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kufanikiwa kukamata magari 15 yaliyokuwa yakitumia namba za usajili zisizo rasmi za “SSH 2530”.
Magari hayo yalibainika kuendeshwa bila usajili halali, kinyume na Kifungu cha 13(i) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura 168 ya mwaka 1973, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
Aidha, Murilo alieleza kuwa mnamo 11 Agosti 2025, polisi walimkamata Ramadhan Makala, dereva mkazi wa Tabata, akitumia gari aina ya Fuso (T 733 AGT) kusafirisha bangi iliyochanganywa na magunia ya mahindi na mchele. Katika msako huo, jumla ya magunia 13 ya bangi yenye uzito wa kilo 239 yalipatikana.
Kwa sasa, mtuhumiwa huyo na wenzake wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika.
Katika oparesheni nyingine, kati ya 12 hadi 20 Agosti 2025 eneo la Magomeni, jeshi la polisi liliwakamata watuhumiwa wawili – Hassan Hamis (mkazi wa Tandale) na Elia Maponda (mkazi wa Goba) – kwa kuhusishwa na mtandao wa wizi wa pikipiki sita na injini mbalimbali za vyombo vya usafiri jijini Dar es Salaam.
Murilo alisema uchunguzi unakamilishwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtandao huo, ambao umekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Kamishna huyo alizungumzia pia vitendo vya ukatili vilivyotokea katika maeneo ya Ilala, Temeke na Kinondoni, ambapo baadhi ya watuhumiwa wa kesi za ulawiti na ubakaji tayari wamekamatwa na mashauri yao yanaendelea mahakamani.
Miongoni mwa waliotiwa hatiani ni: Bashiru Selemani (Kivule) – miaka 30 jela, Tyson Fidel Malingumu (Chanika) – miaka 30 jela, Nicholas Gabriel Thomas (Tabata Barakuda) – kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka na kulawiti.
Murilo aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mapema ili kuzuia vitendo vya kikatili kabla havijatokea.
Akizungumzia maandalizi ya Sikukuu ya Maulid kesho, 5 Septemba 2025, Murilo alisisitiza kuwa jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha usalama wa watu wote.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha familia zao, mali, na nyumba zao zinakuwa salama, akihimiza angalau mtu mmoja kubaki nyumbani wakati wengine wakisherehekea, ili kudhibiti matukio ya wizi wa vifaa vya kielektroniki kama redio, simu na televisheni.
Polisi pia wamewataja watuhumiwa wa uvunjaji nyumba kuwa ni Hussein Ally (Tandale), Razaki Ramadhani (Manzese), na Gift Shabani (Kimara).
Murilo alitoa tahadhari kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata uangalizi maalum wakati wa misongamano ya watu, ili wasipate madhara au kuingia mikononi mwa watu wenye nia ovu.
Aidha, aliwakumbusha madereva kuzingatia sheria za barabarani na kuepuka uzembe unaoweza kuhatarisha maisha.
Akihitimisha mkutano huo, Murilo aliwatakia Watanzania wote amani na utulivu wakati wa kusherehekea sikukuu ya Maulid, akisisitiza kuwa jeshi la polisi litaendelea kusimamia sheria na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

