Breaking News

CCK: Mikopo nafuu, Afya bora na Ajira kwa vijana


Na Kelvin Kijo 

Shamrashamra, nyimbo na vifijo vimetawala leo tarehe 3 Septemba 2025 katika viwanja vya Manzese, jijini Dar es Salaam, wakati Chama cha Kijamii (CCK) kikimtambulisha rasmi mshika bendera wake wa kugombea urais, David Daudi Mwaijojele. Tukio hilo lilihudhuriwa na mamia ya wafuasi na wanachama wa chama hicho, waliokusanyika kushuhudia mwanzo wa safari ya kisiasa ya kuelekea Ikulu.

Mwaijojele alipanda jukwaani na kuanza hotuba yake kwa maneno ya shukrani:

“Namshukuru Mungu kutuwezesha kuwepo mahali hapa, pamoja na Rais Samia na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuunganisha vyama vya siasa vifanye kampeni za ushindani. Pia nashukuru kwa gari jipya nililopewa kwa ajili ya kampeni.”

Katika hotuba yake, Mwaijojele alisisitiza dhamira ya CCK kuondoa changamoto za wananchi wa hali ya chini, wakiwemo mama lishe na wafanyabiashara wadogo, kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kufanya kazi.


Miongoni mwa sera alizozinadi ni:

1.Mikopo nafuu yenye riba ndogo ili kudhibiti ukopeshaji wa "kausha damu".

2.Kila nyumba nchini kupata milo mitatu kwa siku.

3.Kuondoa urasimu na kero za gharama za kuhifadhi maiti hospitalini.

4.Huduma bora za afya kwa wote.

5.Uwekezaji mkubwa katika rasilimali za taifa, ajira kwa vijana wasomi, na mafao bora kwa wastaafu.

6.Kuwawezesha wavuvi kupata meli kubwa za kisasa kwa ajili ya uvuvi.

“Utaona mabadiliko makubwa katika jamii CCK ikikamata dola ya Tanzania,” alisema kwa kujiamini.

Mbali na mshika bendera wa urais, wagombea wengine wa nafasi mbalimbali za ubunge na udiwani nao walipata nafasi ya kueleza sera na matarajio yao:

Devota Nalungu (Ubungo): Aliahidi kusikiliza na kutatua kero za wananchi, akimalizia hotuba yake kwa maneno mafupi: “Naomba kura zenu tarehe 29 Oktoba.”

Emmy Hudson Mwakisole (Jimbo la Kibamba): Alisisitiza kuwa CCK ni chama kinachoshughulikia matatizo kuanzia familia hadi taifa, kwa kuhakikisha watoto wanasoma, wananchi wanapata lishe bora na huduma za afya.

Mariam Dastan Mkande (Jimbo la Kinondoni): Aliahidi kutatua kero za wajane, watoto mashuleni na kuondoa urasimu hospitalini.

Michael Lugendo (Kata ya Manzese): Aliahidi barabara za kisasa, soko bora la Manzese na maendeleo ya kweli.

Asnati Samweli (Kata ya Mabibo): Aliwaomba wananchi kuipigia kura CCK katika nafasi zote za urais, ubunge na udiwani.

Chama cha Kijamii (CCK) kilianzishwa mwaka 2012, na katika uchaguzi huu kimepeleka wagombea katika majimbo na kata kote nchini Tanzania. Kauli mbiu yao ya kampeni ni:

“Mabadiliko ni Sisi, Tunachukua Dola.”