GCAP TANZANIA WAADHIMISHA MIAKA KUMI YA MAENDELEO ENDELEVU YA DUNIA ( SDGs)
Na Hawa Ismail- Dar es Salaam
Katika kuadhimisha miaka kumi ya utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs), Mratibu wa Taifa wa Shirika la Sahringon Tanzania Chapter na GCAP Tanzania Coalition, Bi Martina Kabisama, amesisitiza umuhimu wa kupanua elimu ya msingi, kuboresha huduma za afya, na kuimarisha miundombinu kama hatua muhimu za kupambana na umaskini duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Septemba 25, 2025, Bi Kabisama alieleza kuwa dira ya maendeleo ya Tanzania kwa kipindi cha 2025 hadi 2050 inalenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu. Aliongeza kuwa dira hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wastani wa zaidi ya asilimia 8, kuongeza umri wa kuishi hadi miaka 75, na kuhakikisha kaya zaidi ya asilimia 90 zinapata huduma ya nishati.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana na mipango madhubuti ya maendeleo, bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo kiwango kikubwa cha umasikini, ukosefu wa ajira kwa vijana, kutokuwepo kwa usawa wa kijamii, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala ya uongozi na uwajibikaji,” alisema Bi Kabisama.
Kwa upande wake, Bi Rosemary Mwaipopo kutoka Global Call to Action Against Poverty (GCAP) alitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuhakikisha inalinda haki za raia, kuimarisha misingi ya haki za binadamu, kusimamia utawala bora, na kuongeza uwekezaji katika ulinzi wa jamii. Alisisitiza kuwa sera na bajeti za kitaifa zinapaswa kuelekezwa katika kujenga uchumi jumuishi na kutoa ajira zenye staha kwa vijana.
Katika hatua nyingine, Bi Mwaipopo aliwahimiza wadau wa maendeleo, sekta binafsi, Umoja wa Mataifa, taasisi za kikanda na asasi za kiraia kuendelea kupaza sauti za wananchi—hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu—ili kuharakisha utekelezaji wa SDGs nchini Tanzania.
