WAWEKEZAJI WAITWA KUWEKEZA SINGIDA NA DODOMA
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Mikoa ya Singida na Dodoma ina fursa nyingi kwenye kilimo ,viwanda pamoja na ufugaji ikiwemo Ufugaji wa Nyuki hivyo wawekezaji wameaswa kuwekeza Katika mikoa hiyo Ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Nchi.
Hayo ameyasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalum ya kiuchumi (TIZESA) Gilead Teri wakati anazungumza na waandishi wa habari katika mwendelezo wa maonesho ya wakulima, Nanenane yanayofanyika Zunguni Jijini Dodoma huku akibainisha kuwa ushiriki wao wa kongamano la uwekezaji la Kanda ya kati umelenga kuhabarisha Umma kuhusu fursa zinazopatina Katika Mikoa hiyo.
Pia Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kongamano hilo lililenga kufanya utambulisho wa TIZESA upya kwa wawekezaji wa Kanda ya kati na kutoa habari njema ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amewapa jukumu la kuwa kituo cha pamoja cha uwekezaji.
Aidha amesema Kuwa tarehe 12 Agosti Mwaka huu watazindua huduma mpya za uhamasishaji na uwekezaji ndani ya TIZESA ambapo wataanza na maeneo (5) ambayo ni pamoja na Benjamin mkapa Dar- Es- Salaam, Bagamoyo hekari 150, Kwala hekari 100 Dodoma hekari 600 pamoja na Buzwagi ambapo wanatarajia utazinduliwa na waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.
Naye mwakilishi msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Charles Tulahi amesema kuwa Wanaratibu miradi mbalimbali nchini Tanzania ambapo kwa Dodoma wanawezesha wanawake kiuchumi.
Kati ya mradi wanaoutarajia kuanzishwa ni pamoja na kilimo cha tende Mkoani Dodoma hivyo wakulima wa sekta mbalimbali watawekeza na kuleta mageuzi kwasababu tende zilikuwa zinaagizwa kutoka nje.
Hata hivyo Tulahi amewaasa watanzania kuwekeza katika kilimo katika sehemu mbalimbali zenye mnyororo wa thamani kwasababu Duniani kote idadi ya watu imekua na uhitaji wa Mazao ya kilimo pia yamekua hivyo uwekezaji kwenye kilimo unatija kubwa.

