Breaking News

Vyombo vya Habari Vyaaswa Kulinda Amani Kipindi cha Uchaguzi

Mkurugenzi Mkuu, INEC Ndg. Ramadhani Kailima akiongea wakati wa kufungua mafunzo siku ya tatu ukumbi wa Mlimani City, 04 Julai 2025
Vyombo vya habari vimetakiwa kuzingatia maadili ya uandishi na kulinda amani ya taifa katika kipindi cha uchaguzi kwa kuepuka taarifa zinazoweza kuchochea chuki au migogoro.

Akizungumza katika mafunzo ya siku tatu kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari leo tarehe 4 Julai 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa INEC, Ramadhani Kailima, amesema tume itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa rasmi kwa wakati na kwa usahihi.

Wahariri na waandishi wa vyombo vya habari wakipokea mafunzo ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam 


Naye Mwakilishi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Egbert Mkoko, amesisitiza umuhimu wa kutoa habari sahihi, zisizo na ubaguzi wala mwelekeo wa kutenganisha taifa.

Dkt. Egbert Mkoko akiendelea na mafunzo kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Utangazaji Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Mhandisi Andrew Kisaka, ameonya dhidi ya kusambaza taarifa za uongo na kutoa majukwaa kwa wachochezi, akisisitiza kupewa kipaumbele sauti za maridhiano na mshikamano wa kitaifa.

Mkurugenzi wa Huduma za Utangazaji, TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka akiwasisitiza wapokea mafunzo 

“toeni vipaumbele kwa sauti zinazoshawishi amani kwa umma na kurejesha utu wa kitanzania kuhusu dhana potofu kuhusu upinzani wao wa kisiasa na mchakato wa uchaguzi” Amesema Mhandisi Kisaka.

Aidha katika kuangazia uchapishaji wa taarifa binafsi za watu Mkuu wa Mawasiliano Serikalini katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Innocent Mungi amewataka waandishi kuwa na sera thabiti za kushughulikia taarifa za faragha na kutumia teknolojia kwa uangalifu chini ya uamuzi wa mhariri mkuu.

Ndg. Innocent Mungi akifundisha maswala ya faragha na matumizi sahihi ya akili mnemba (AI)

“iweni na sera za kushughulikia maswala ya faragha na taarifa binafsi na kuwaweka wazi walengwa kufahamu namna taarifa zao zitavyotumiwa”. Ameongezea kuwa matumizi ya teknolojia na akili mnemba yatumiwe kwa utashi wa mhariri na ndio awe mtu wa mwisho kuruhusu taarifa sinazofika kwa umma."

Akihitimisha, Mtibora Selemani kutoka INEC, amewahimiza waandishi kufahamu vyema taratibu za uchaguzi na kuzingatia wajibu wao bila kuvuruga mchakato huku akihakikishia Tume ya Huru ya Uchaguzi itakuwa karibu kushirikiana na vyombo vya habari katika kipindi chote cha Uchaguzi.

Mwakilishi wa Tume Huru ya Uchaguzi INEC, ndugu Mtibora Selemani