Breaking News

TANZANIA YASISITIZA AMANI NA UTULIVU KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025


Na Kelvin Kijo

Dar es Salaam, 20 Agosti 2025 – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamza Hassan Juma, akimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Hemedi Suleiman Abdalla, ametuma salamu za pongezi kwa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) na Global Peace Foundation Tanzania (GPF) kwa kuandaa mdahalo wa kujadili mikakati ya kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akihutubia mdahalo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Waziri Hamza alisema Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani barani Afrika.

“Amani ya taifa la Tanzania imeshawishi hata nchi jirani zilizopitia changamoto za usalama kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mwalimu Julius Nyerere na Rais Abeid Karume waliweka msingi wa mshikamano kwa kuondoa tofauti za kidini, na amani hiyo inaendelea kuishi hadi leo.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Murilo, alisisitiza kwamba jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa haki na usalama.

“Tunafahamu kuwa tarehe 29 Oktoba 2025 Tanzania itafanya uchaguzi. Hatutasubiri vitendo vya kihalifu vitokee. Jeshi letu litafanya kazi kwa bidii, weledi, haki na utulivu mkubwa ili kulinda amani na kuzuia machafuko.”

Aliongeza kuwa jeshi la polisi litahakikisha wapigakura, wasimamizi wa uchaguzi na kura zinalindwa kwa usawa, bila vitisho wala ubaguzi.

Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayoub Rioba, aliwataka wanahabari kutumia kalamu zao kujenga demokrasia.

“Vyombo vya habari vinapaswa kuwa walimu wa demokrasia, si chombo cha propaganda au taarifa za utapeli. Ni wajibu wetu kutumia teknolojia kuelimisha Watanzania kuhusu haki zao na umuhimu wa amani.”


Mwakilishi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ally Ahmed, alisema taasisi yake imekuwa ikiendesha semina na mikutano ya pamoja kwa lengo la kuongeza mshikamano:

“Hatuviachi vyama vya siasa vitangetange bila mwongozo. Tunavileta pamoja, tunajadili changamoto na kuhakikisha mshikamano miongoni mwa washiriki wa uchaguzi.”


Rais wa Jopo la Masheikh Tanzania, Sheikh Abdallah Ndauga, alisisitiza nafasi ya viongozi wa dini katika kutuliza joto la kisiasa na kudumisha mshikamano wa kitaifa.

“Wajibu wetu ni kuzungumza na wananchi wapate utulivu wa akili, wakubaliane na matokeo pasipo chuki, huku tukimwomba Mungu alinde mioyo yao kutetea amani ya nchi.”


Mwenyekiti wa JMAT mkoa wa Dar es Salaam, Mch. Christosiler Petro Kalata, alieleza kwamba jumuiya yake ina jukumu la kuunganisha wananchi katika subira, huruma na mshikamano wa kitaifa.

“Tunazidi kuonya dhidi ya vitendo vya kuaibisha vinavyolenga kuharibu sifa za wagombea. Ni jukumu letu kuwakumbusha Watanzania kuwa na moyo wa kutanguliza amani ya taifa kabla ya maslahi binafsi.”