KILA MTANZANIA KUELEKEA KIPATO CHA MILIONI 18 KWA MWAKA – DIRA 2050
Na Kelvin Kijo
Dar es Salaam, Agosti 2025 – Tume ya Taifa ya Mipango (NPC) imetangaza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaanza rasmi mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kujenga taifa lenye maendeleo jumuishi na endelevu.
Akizungumza wakati wa kikao cha wadau jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mtendaji wa NPC, Bw. Brusali Milanzi, alisema maandalizi ya utekelezaji wa dira hiyo yako katika hatua za mwisho, ikiwemo kuandaa Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano (2026 – 2031) ambao utakamilika mwezi Novemba mwaka huu.
“Tumeanza kwa kuandaa mpango wa miaka mitano utakaokuwa wa kwanza katika utekelezaji wa Dira 2050. Kupitia mpango huu, wizara zote zitapata mwongozo wa kimkakati na kutekeleza mipango ya mwaka kwa kupitia bajeti ya serikali kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027. Lengo letu ni kuelekea ‘kaskazini’, yaani maendeleo ya kweli kwa taifa letu, hadi tufikie malengo tuliyojiwekea ifikapo mwaka 2050,” alisema Bw. Milanzi.
Miongoni mwa malengo makuu ya dira hiyo ni kuhakikisha kila Mtanzania anafikia kipato cha wastani wa dola za Marekani 7,000 kwa mwaka (takriban shilingi milioni 18.27), sawa na zaidi ya shilingi 1.5 milioni kwa mwezi.
Bw. Milanzi alibainisha kuwa utekelezaji wa dira hii utahusisha uwajibikaji wa kitaasisi na sekta zote, ili kila wizara na taasisi iwasilishe mpango unaoendana na mwelekeo wa Dira ya 2050.
“Tunataka kila Mtanzania aweze kueleza kwa vitendo namna anavyoshiriki katika utekelezaji wa dira hii. Hii inahusu kila mmoja – iwe ni bodaboda, mkulima, mjasiriamali, mfanyakazi wa afya, au sekta ya teknolojia. Dira hii siyo ya serikali pekee, bali ni safari ya pamoja ya taifa lote,” aliongeza.
Kwa upande wake, Melissa McNeil-Barrett, Naibu Mwakilishi Mkazi na Kaimu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), aliuelezea waraka wa Dira 2050 kama “nyenzo shupavu na ya kimkakati” itakayoipeleka Tanzania kwenye maendeleo jumuishi na endelevu.
“Dira hii inaleta uwajibikaji wenye maana kwa kila Mtanzania. Tunaamini Tanzania itafanikisha malengo yake ya muda mrefu ifikapo mwaka 2050,” alisema McNeil-Barrett.
Aidha, Samwel Elisa Msokwa, Msimamizi wa Kitengo cha Idadi ya Watu na Maendeleo wa UNFPA, alibainisha kuwa shirika hilo limeendelea kushirikiana na serikali katika nyanja za takwimu, sensa na tafiti za kijamii, hususan kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Julai 2025, na sasa maandalizi ya utekelezaji wake yanaanza kutekelezwa kwa kasi.




