Majaliwa: TRAMPA ni Injini ya Taifa Kufanikisha Dira ya 2050
![]() |
| Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiteta jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, 27 Agosti 2025, Diamond Jubilee-DSM |
Na Kelvin Kijo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo tarehe 27 Agosti 2025 amezindua Mkutano Mkuu wa 13 wa Wataalamu wa Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema TRAMPA ni injini ya Taifa katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya 2050, akizitaka taasisi zote kujiunga na mfumo wa E-Office ili kuongeza kasi ya utendaji na kulinda urithi wa Taifa. “Punguzeni matumizi ya karatasi na ongezeni ubunifu katika utunzaji wa kumbukumbu kwa njia ya Ofisi Mtandao,” alisema Majaliwa.
Katika risala yake, Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devota George Mrope, aliitaka serikali kuongeza mafunzo kwa watumishi wa masijala na kuwekeza zaidi kwenye vifaa vya kisasa vya kuhifadhi kumbukumbu. Pia aliiomba serikali kuruhusu Mwenge wa Uhuru kukagua ofisi za masijala kote nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora (SMZ), Mhe. Mwl. Haroun Suleiman, alitangaza mchango wa TZS milioni 10 kwa ujenzi wa Kituo cha Maarifa, huku Waziri George Simbachawene akieleza kuwa serikali imeajiri watumishi 965 na kupandisha vyeo 1,237 wa sekta hiyo, sambamba na kuchangia TZS milioni 10 kwa mradi huo.
Sherehe hiyo pia iliambatana na utoaji wa tuzo kwa taasisi mbalimbali zikiwemo TRA, TCRA, TBA na Wizara ya Fedha, pamoja na TRAMPA kumkabidhi Waziri Mkuu gari jipya la kusafirisha wagonjwa, na mama wajawazito kwa heshima ya Rais Samia Suluhu Hassan.
TRAMPA, iliyoanzishwa mwaka 2012 na kusajiliwa mwaka 2014, imeongeza wanachama wake kutoka 4,500 mwaka 2023 hadi 8,000 mwaka 2025. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Matumizi ya Ofisi Mtandao ni Chachu ya Kufikia Malengo ya Dira ya 2050.”
![]() |
| maelfu ya wanachama wa TRAMPA kutoka kanda zote Tanzania wakiwa kwenye tukio la uzinduzi |
![]() |
| Waziri Simbachawene akimkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa ufunguo wa gari la wagonjwa (ambulance) |
![]() |
| Waziri Mkuu Majaliwa akijadili jambo na Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi Devota Mrope meza kuu wakati uzinduzi |



