CUF Kufanya Mkutano Mkuu Maalum Kupitisha Wagombea wa Urais
Hawa Ismail- Dar es Salaam
Chama Cha Wananchi (CUF) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu Maalum kesho, Agosti 9, 2025, kwa ajili ya kupitisha wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, waliopendekezwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho lililokutana Agosti 6 mwaka huu.
Taarifa hiyo imetolewa leo, Agosti 8, 2025, na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba alibainisha kuwa wagombea waliopendekezwa kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Gombo Sambandito Gombo na Nkunyuntila Siwale.
Kwa upande wa Zanzibar, waliopendekezwa kugombea nafasi ya urais ni Mhandisi Mohamed Habib Mnyaa, Mhandisi Hamad Masoud Hamad, na Dkt. Mohamed Habib Mikidadi. Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum watapiga kura kumchagua mgombea mmoja atakayewakilisha CUF katika kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Profesa Lipumba aliongeza kuwa kupitia mkutano huo, CUF itazindua rasmi Ilani ya Uchaguzi kwa ajili ya kutangaza sera za chama kwa wananchi, ili kuwajengea imani na kuwashawishi wakipe ridhaa ya kuongoza dola.
"Baraza Kuu la Uongozi Taifa limepokea na kupitisha rasimu ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu kwa upande wa Muungano na Zanzibar, pamoja na kupitisha wagombea wa Ubunge na uwakilishi," alisema Profesa Lipumba.
Alifafanua kuwa Ilani ya CUF imebeba maono mapana ya kujenga Tanzania Mpya kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye misingi ya usawa, mshikamano, uwajibikaji, demokrasia ya kweli, na maendeleo jumuishi kwa watu wote.
"Ilani ya CUF imejikita katika kuleta haki sawa na furaha kwa wananchi wote, kujenga uchumi jumuishi unaoongeza ajira na kuondoa umasikini, kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala wa sheria kwa kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi, na kuweka msingi wa maendeleo endelevu kwa kufanikisha malengo ya SDGs ifikapo mwaka 2030," alieleza Profesa Lipumba.
Aidha, aliongeza kuwa Ilani hiyo inatekeleza sera ya CUF ya kipato cha msingi kuwa haki ya kila Mtanzania, kwa kuanza kuwalipa wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea kipato cha msingi cha kujikimu. Alisisitiza kuwa iwapo uchaguzi mkuu utakuwa huru na wa haki, wagombea wa CUF watapata ushindi.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alieleza kuridhishwa kwake na mabadiliko yaliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikiwemo hatua ya kuvikabidhi vyama vya siasa nakala halisi za Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Alisema hatua hiyo itawasaidia mawakala kutambua idadi na majina kamili ya wapiga kura katika vituo vya kupigia kura.
