TIRA na DSE waingia mkataba wa kimkakati kuchochea ukuaji wa kiuchumi
Na Hawa Ismail, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeingia makubaliano ya maridhiano (MoU) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa lengo la kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi nchini Tanzania.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Julai 31, 2025, jijini Dar es Salaam, yakilenga kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya bidhaa bunifu za kifedha. Bidhaa hizo ni pamoja na huduma za bima zinazoweza kuorodheshwa sokoni, pamoja na kukuza elimu ya fedha kwa umma na kuboresha uwazi, uwajibikaji na usawa wa taarifa kati ya TIRA na DSE.
Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware, amesema makubaliano hayo si tu hati ya ushirikiano, bali ni hatua ya ujasiri na ya kimkakati katika kuunganisha sekta ya bima na masoko ya mitaji na dhamana, ambazo ni sehemu muhimu ya sekta ya fedha nchini.
"Makubaliano haya yatakuwa dira ya jinsi sekta hizi mbili zitakavyofanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa Watanzania wote, na kuchochea kasi ya mabadiliko ya ukuaji wa kiuchumi sambamba na nguzo za Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050," alisema Dkt. Saqware.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Bw. Peter Situmbeko Nalitolela, alieleza kuwa mkataba huo utawezesha usajili na utoaji wa leseni kwa watoa huduma za bima, kuandaa kanuni na miongozo ya kusimamia soko la bima, pamoja na kulinda haki za wateja, kutoa elimu ya bima kwa umma na kuishauri serikali kuhusu masuala ya sekta hiyo.
"Makubaliano haya yatasaidia kuboresha mifumo ya taarifa kwa ajili ya usimamizi na uchambuzi wa taarifa za kifedha, na pia kuwezesha kampuni za bima kuchangia kwenye soko la mitaji kwa kuorodhesha dhamana zao. Hatua hii itachangia kukuza mtaji wa ndani na kuimarisha uwezo wa kifedha wa taasisi," alisisitiza Bw. Situmbeko.
Aidha, makubaliano haya yanatarajiwa kufungua sura mpya ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili, ukiwa na malengo ya kuelimisha jamii, kuhimiza uwajibikaji na kurahisisha upatikanaji wa mitaji. Hatua hii inatarajiwa kuleta manufaa kwa wananchi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, taasisi hadi uchumi wa Taifa kwa ujumla.



