RAIS SAMIA KUPOKEA MABEHEWA MAPYA YA MIZIGO NA KUZINDUA BANDARI KAVU YA KWALA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Bandari ya Kwala pamoja na kupokea jumla ya mabehewa mapya 50 ya mizigo pamoja na mabehewa 20 yaliyofanyiwa ukarabati siku ya tarehe 31 Julai 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, alibainisha kuwa hafla hiyo pia itahusisha uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kuanza kwa safari rasmi ya treni ya mizigo kupitia reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Prof. Mbarawa alisema lengo kuu la kuanzishwa kwa treni ya mwendo kasi ni kukuza biashara, hasa kwa kusafirisha mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa haraka na ufanisi. Aidha, alieleza kuwa safari za SGR zitapanuliwa hadi nchi jirani kama Burundi na DRC, hatua ambayo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
"Rais Samia, wakati akifunga shughuli za Bunge jijini Dodoma, alieleza kuwa serikali inaendelea na uboreshaji wa reli ya kati ili iendelee kutoa huduma pamoja na reli mpya ya SGR, kwa kuhakikisha zote zinatumika kikamilifu," alisema Prof. Mbarawa.
Kuhusu faida za Bandari Kavu ya Kwala, Prof. Mbarawa alifafanua kuwa bandari hiyo itaongeza ufanisi wa usafirishaji kutokana na kupanuka kwa shehena inayopitia Bandari ya Dar es Salaam. Pia, itaongeza mapato ya serikali, kupunguza gharama za usafirishaji, na kuvutia wafanyabiashara wengi, sambamba na kukuza shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Dar es Salaam.
Vilevile, aliongeza kuwa Bandari ya Kwala itasaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara, kuchochea ongezeko la ajira kwa wakazi wa eneo hilo, na kufungua fursa za viwanda.
Katika hatua nyingine, usafirishaji wa mizigo kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utapunguza muda wa safari kutoka masaa 12 hadi masaa manne, kuhakikisha usalama wa mizigo, na kupunguza athari za kimazingira.
Prof. Mbarawa alieleza kuwa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia SGR ulianza rasmi tarehe 27 Juni 2025 kwa kusafirisha makontena 10 ya bidhaa mchanganyiko zenye uzito wa tani 700 kutoka kampuni ya Azania. Tarehe 9 Julai 2025, makontena 20 yenye tani 1,400 za saruji kutoka kampuni ya Dangote yalisafirishwa. Shirika la Reli Tanzania (TRC) lina mpango wa kuongeza mabehewa ya mizigo hadi kufikia 30, kwa uwezo wa kubeba hadi tani 210,000.
