Breaking News

TAMWA Yawahamasisha Wahariri Kuandika Habari Kuhusu Afya ya Uzazi

Dkt. Rose Reuben (Mkurugenzi - TAMWA) akiongea na wahariri kuhusu Afya ya Uzazi na Haki Zake wakati wa mafunzo Dar es Salaam

Na Kelvin Kijo, Dar es Salaam 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeendesha mafunzo ya siku moja leo jijini Dar es Salaam kwa wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika kuripoti masuala ya afya ya uzazi na haki zake (SRHR).


Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amewataka wahariri kuwa mstari wa mbele katika kuandika habari za kina kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake, wanaume na watoto katika masuala ya afya ya uzazi, kwa kushirikiana na taasisi kama Marie Stopes, UNFPA, TGNP na Engender Health.


“Haki ya afya ya uzazi ni pamoja na kupata taarifa sahihi. Vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuzipeleka taarifa hizi kwa mamlaka husika,” alieleza Dkt. Reuben.


Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Syriacus Buguzi, aliwasisitiza wahariri kuhakikisha taarifa za SRHR zinawasilishwa kwa lugha rahisi, sahihi na isiyopotosha. “Habari inapaswa kueleweka kwa jamii na kuzingatia ukweli wa kisayansi,” alisema.