Breaking News

Katetu Aishukuru INEC kwa Mafunzo ya Vitendo ya Uchaguzi Yaliyoimarisha Uwezo wa Wasimamizi


 Na Hawa Ismail, Dar es Salaam 

Mwenyekiti wa mafunzo ya uchaguzi, Ndugu Selemani Katetu, ameishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kuwawezesha washiriki kupitia mafunzo ya kina ya vitendo katika nyanja mbalimbali za uchaguzi. Katika mafunzo hayo, jumla ya mada zaidi ya 11 zilifundishwa kwa lengo la kuboresha uelewa na utendaji wa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi zote.


Miongoni mwa mada zilizotolewa ni majukumu ya watendaji wa uchaguzi, uteuzi wa wagombea, maadili ya kampeni na ya wagombea, jukumu la mawakala, pamoja na mazoezi ya ujazaji wa fomu, upokeaji wa vifaa vya uchaguzi, na utaratibu wa upigaji kura. Katetu alieleza kuwa washiriki waliweza kuona video za mifano na kufanya mazoezi ya kutosha, hatua iliyowawezesha kuelewa kwa vitendo majukumu yao na kufanya kazi kwa ubora zaidi kipindi cha uchaguzi.


Aliongeza kuwa washiriki walijifunza utaratibu wa kuhesabu kura vituoni, kupiga kura, pamoja na kupitia sheria za uchaguzi, gharama za uchaguzi, na kampeni. Mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kuwawezesha wakufunzi katika ngazi ya kata na wasimamizi wa vituo, kwa kuzingatia kwa makini miongozo iliyotolewa.


Akihutubia washiriki wenzake, Katetu aliwakumbusha kuwa wamepewa dhamana kubwa ya kitaifa, akisisitiza kufanya kazi kwa uzalendo, haki, na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao ya uchaguzi.


Kwa upande wake, Balozi Omar Ramadhan Mapuri alibainisha kuwa lengo la mafunzo ya siku tatu ni kukumbushana majukumu ya tume, wajibu wa usimamizi na uendeshaji wa uchaguzi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kujifunza sheria mpya za uchaguzi wa mwaka 2024, ikiwemo Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Wabunge na Madiwani, na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.



"Alieleza kuwa maeneo mapya ya kisheria yanayohusu wapiga kura wa Rais walioko nje ya vituo walivyojiandikisha, hali ya kuwepo mgombea mmoja, na kura zinazopigwa magerezani ni miongoni mwa vipengele vilivyokuwa havipo hapo awali na vinahitaji uelewa wa kipekee" alisema Balozi Omar Mapuri 


Vilevile, Barozi Omar Ramadhan Mapuri alibainisha kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kwa weledi wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya kata kusimamia masuala yote ya uchaguzi. Hii ni pamoja na kuanza vikao na vyama vya siasa, utoaji wa fomu za uteuzi, uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, na kuhakikisha uteuzi unafanyika kwa mujibu wa sheria.


Alisisitiza umuhimu wa kuandaa kamati za ratiba za kampeni na maadili, hususan pale kutakapojitokeza changamoto wakati wa kampeni. Pia aliwakumbusha wajibu wa ubandikaji wa mabango, matangazo, na orodha za majina kwa kufuata kalenda ya uchaguzi ili kuepusha malalamiko na vurugu.


Katika hitimisho lake, alitoa ombi kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha taarifa zinazotolewa kwa vyombo vya habari zinashirikishwa na kujadiliwa kwa pamoja kabla ya kutolewa rasmi, ili kuepusha migogoro na kuhakikisha utulivu katika maeneo yao ya kazi na taifa kwa ujumla. Pia aliwakumbusha kuzingatia kiapo cha utunzaji siri, akieleza kuwa uvunjaji wa kiapo hicho ni kosa linaloweza kupelekea uwajibikaji wa kisheria.