BILIONI 1.5 ZIMETOLEWA KWA AJILI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MIFUGO KATAVI
Na. Wellu Mtaki, Dodoma
Serikali Katika kuhakikisha Sekta ya Mifugo Mkoa wa katavi unafikia Malengo yake imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za mifugo ikiwemo majosho, mabirika, malambo, vibanio sambamba na kusambaza dawa za kuogesha mifugo zenye ruzuku ya serikali katika majosho yote yanayofanya kazi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya sita wa Mkoa huo.
Amesema mafanikio ya ujenzi wa miundombinu hiyo imesaidia Kupungua kwa milipuko ya magonjwa ya wanyama kutoka asilimia 72 mwaka 2021 hadi asilimia 15 mwaka 2025 pamoja na Kuweka mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na kuanzisha viwanda vya vyakula vya mifugo .
"Bilion1.5 zimetolewa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za mifugo ikiwemo majosho, mabirika, malambo, vibanio na sambamba na kusambaza dawa za kuogesha mifugo zenye ruzuku ya serikali katika majosho yote yanayofanya kazi. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na;-(a) Kupungua kwa milipuko ya magonjwa ya wanyama kutoka asilimia 72 mwaka 2021 hadi asilimia 15 mwaka 2025; (b) Kuweka mazingira wezeshi ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na kuanzisha viwanda vya vyakula vya mifugo ambapo kwa kushirikiana na sekta binafsi kumeanzishwa viwanda viwili vya kuchakata vyakula vya mifugo pamoja na viwanda vya maziwa ikiwemo kiwanda cha MSS Fresh Milk" Amesema Mrindoko
Aidha amesema kuwa ongezeko la vituo161 kwa Mwaka huu na vituo vilivyoboreshwa vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharura ya upasuaji kwa kina mama wajawazito kutoka vituo 8 Mwaka 2021 hadi kufikia vituo 14 Mwaka 2025 ambapo Ongezeko hilo limeweza kusaidia wakina Mama wajawazito 48,322 kujifungua.
"kumekuwa na ongezeko la vituo vilivyoboreshwa vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharura ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji kwa kina mama wajawazito kutoka vituo 8 Mwaka 2021 hadi kufikia vituo 14 Mwaka 2025, Aidha, Wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya huduma wameongezeka mwaka hadi mwaka. Kina mama 40,269 mwaka 2021 hadi kufikia kina mama 48,322 mwaka 2025" amesema Mrindoko.
Pia ameeleza kuwa Mkoa unaendelea kutekeleza mradi wa usamabazaji Maji kutoka Bwawa la Milala unaotekelezwa chini ya mpango wa ujenzi wa mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo Mradi huo unatarajiwa kuzalisha Maji lita 12,000,000 kwa siku na kunufaisha wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda.
"Katika kipindi cha uongozi wa Rais wa awamu ya Sita, Mkoa umeendelea kutekeleza miradi MITANO yenye thamani ya Shilingi bilioni 32,163,080,399.89 ambayo ikikamilika itaongeza upatikanaji wa Maji kwa zaidi ya asilimia 100. Mkoa unaendelea kutekeleza mradi wa usamabazaji Maji kutoka Bwawa la Milala unaotekelezwa chini ya mpango wa ujenzi wa mradi wa Maji wa Miji 28. Mradi huu unatarajiwa kuzalisha Maji lita 12,000,000 kwa siku na kunufaisha wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda. Hadi kufikia Juni, 2025 hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 42 mradi unatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kuanzia 11 Aprili, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Oktoba 2025.5.2 Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira " amesema Mrindoko .


